KESI MAUAJI YA BILIONEA MSUYA: Mshtakiwa: Niliteswa na polisi, nikavunjwa mguu

Mshitakiwa  wa pili katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa Madini ya Tanzanite Erasto Msuya, Shaibu Jumanne alimaarufu Mredii akitoka katika Chumba cha Mhakama Kuu kanda ya Moshi jana,baada ya kutoa utetezi wake katika kesi inayokabili yeye na wa shitakiwa wenzake 5. Picha na Dionis Nyato.

Muktasari:

Jumanne ambaye ni shahidi pekee wa utetezi kwa upande wake, alidai aliamua kuchukua uamuzi wa kumpa talaka moja mkewe aliyemtaja kuwa ni Zuhura Hassan.

Moshi. Mshtakiwa wa pili, Shaibu Jumanne, maarufu kwa jina la Mredii katika kesi ya mauaji ya Erasto Msuya jana alitoa madai mahakamani akisema aliteswa na polisi hadi kupewa ulemavu, ikiwamo kuhasiwa.

Jumanne ambaye ni shahidi pekee wa utetezi kwa upande wake, alidai aliamua kuchukua uamuzi wa kumpa talaka moja mkewe aliyemtaja kuwa ni Zuhura Hassan.

Akiongozwa na wakili Majura Magafu kutoa utetezi, mshtakiwa alidai mbali na kuhasiwa, polisi walimvunja mara mbili mguu wa kushoto na mara moja mguu wa kulia.

Mshtakiwa huyo alidai siku ya mauaji, hakuwapo Arusha wala Kilimanjaro, bali alikuwa shambani Babati akivuna mazao yake, kuanzia Julai 13 hadi Agosti 7, 2013 aliporudi Mirerani.

Shaibu alidai alikamatwa na polisi baada ya kuitwa na mkuu wa kituo cha polisi (OCS) Mirerani, Ally Mkalipa Agosti 17, 2013 saa mbili usiku, na siku iliyofuata alikabidhiwa kwa polisi wa Moshi.

Alidai kuwa akiwa Mirerani, polisi walimfunga pingu na kumfunga kitambaa machoni na kupakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop na kulazwa kifudifudi hadi kituo cha polisi KIA.

Alidai walipofika hapo, hakuingizwa kituoni bali gari liliegeshwa nje na polisi mmoja alipotaka kumshusha, mwingine alimtaka asimteremshe kwa kuwa kuna mtuhumiwa mwenzake.

Alidai kuwa kutokea kituoni polisi walimfunga pingu mikono na kumuingiza kwenye gari na kumlaza kifudifudi na gari liliondoka kuelekea Arusha hadi Kituo Kikuu cha polisi jijini Arusha.

Mshtakiwa huyo alidai kuwa walipofika kituo cha polisi, askari walimuingiza katika chumba kikubwa na walimtaka kueleza kila kitu kuhusu mauaji ya Msuya.

Alidai kuwa aliwaambia polisi hafahamu chochote na kwamba hakuwapo Arusha wala Kilimanjaro na hapo ndipo walipompeleka Kituo cha Polisi cha Kisongo maarufu kama Guantanamo.

“Waliniambia hatutaki kitu kingine zaidi ya saini yako. Kwa hayo mateso niliyopata hapo kituoni nimekuwa mlemavu. Niliwekwa staili ya mbuzi anayechomwa nikiwa sina nguo,” alidai.

Mshtakiwa aliiomba Mahakama ipokee ushahidi wake alioutoa katika kesi ndani ya kesi Septemba 2, 2013 kama sehemu ya ushahidi wake kuonyesha mateso aliyoyapata hapo Guantanamo.

Hata hivyo, maelezo hayo ya onyo ya mshtakiwa yaliyodaiwa ni ya kukiri kosa aliyolazimishwa na polisi kuyasaini yalikataliwa kupokewa na Mahakama katika hatua ya kesi ndani ya kesi.

Akiendelea kujitetea, mshtakiwa alidai hakuwa anamfahamu mfanyabiashara Joseph Mwakipesile ‘Chussa’ kama maelezo ya kukiri kosa ya mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed yalivyosomwa kortini.

“Sikuwa namfahamu kabisa Chussa zaidi ya kuona biashara zake zikiwa zimeandikwa Chussa Mining. Kwanza yeye kumuona mitaani ni vigumu kwa vile anatembea na walinzi,” alidai.

Pia, alikanusha maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Juma Mangu na wa saba Ally Mjeshi yaliyosomwa mahakamani yakimtaja yeye na washtakiwa walishiriki katika tukio hilo.

Mbali na maelezo hayo, lakini mshtakiwa huyo alikanusha maelezo yaliyomo katika maelezo ya ungamo ya mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa yakidai siku ya mauaji alikuwapo eneo la tukio.

Alipoulizwa na wakili Magafu kuwa anaiomba nini Mahakama, aliiomba imuachie huru kwa vile hakuhusika na mauaji hayo na kesi hiyo imemtia ulemavu.

“Mimi ni mgonjwa. Hii kesi imenitia kilema cha maisha. Mahakama iniachie huru nikawahi matibabu kwa sababu magereza haiwezi. Mpaka sasa naambiwa utumbo ni mbovu na miguu yangu ilivunjika.

“Hayo mengine yakuvunjwa miguu yatapona lakini hilo lingine siwezi kujua kama litapona kwa vile nilihasiwa. Hayo ya kuhasiwa ndiyo ninayosema hayana tiba,” alidai.

Alipoulizwa na wakili wa Serikali, Kassim Nassiri kama ana ushahidi wowote alioupeleka mahakamani kuthibitisha kuwa alitiwa ulemavu na polisi, alidai aliwahi kuleta vyeti vya matibabu gerezani.

Alipoulizwa ilikuwaje amelazwa kifudifudi na kufungwa kitambaa kutoka Mirerani na akajua yuko kituo cha polisi KIA au anaelekea Arusha, mshtakiwa alisema ana uzoefu na barabara hiyo.

Hata hivyo, alipoulizwa kama ni kweli aliweza kujua yuko nje ya kituo kikuu cha polisi baada ya kufungwa kitambaa usoni, alisema alifahamu yuko hapo baada ya kufunguliwa kitambaa.

Akiulizwa swali na mshauri wa mahakama, ni lini alimpa talaka mkewe, mshtakiwa alidai wakati alipomtembelea gerezani alichukua uamuzi huo kwa sababu ya tatizo la kuhasiwa.

Mshtakiwa wa tatu ajitetea

Katika hatua nyingine, mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu alidai kortini kuwa alipewa kipigo na mateso makali na polisi waliomkamata ili asaini maelezo ya onyo ya kukiri kosa hilo.

Akiongozwa na wakili wake, Emmanuel Safari, mshtakiwa huyo alidai alikamatwa Agosti 11, 2013 kati ya saa tano na saa saba usiku, na timu ya polisi iliongozwa na Inspekta Damian Chilumba.

Mshtakiwa huyo alidai baada ya kukamatwa, aliteswa na polisi ikiwamo kupigwa na kitako cha bunduki na kuingiziwa spoku ya baiskeli kwenye uume ili asaini maelezo ya kukiri kosa hilo.

Kwa mujibu wa mshtakiwa, mateso mabaya zaidi aliyapata kituo cha polisi Kisongo ambako aliingiziwa spoku ya baiskeli, na hata alipofikishwa gerezani alikuwa akikojoa damu na usaha.

“Kwa hali niliyokuwa nayo ya kupigwa, kutopewa chakula kwa siku nikaona sina budi kuyasaini maelezo hayo. Baada kusaini hayo maelezo hawakunigusa tena,” alidai mshtakiwa.

Akiongozwa na wakili wake, Emmanuel Safari kutoa ushahidi wake, mshtakiwa huyo alidai Agosti 1, 2013 alisafiri kwenda kumuuguza baba yake huko Singida na kurejea Arusha Agosti 7,2013.

Katika ushahidi wake huo wa msingi, alidai aliondoka Arusha kwa kutumia basi la Mohamed Classic na kurudi kwa basi la Best Line, na tiketi mbili alizokata siku hiyo zilikuwa na majina yake.

Mahakama yaombwa ipokee tiketi

Mangu aliiomba Mahakama ipokee tiketi hizo kama sehemu ya ushahidi wake, lakini mawakili wa Serikali wakiongozwa na wakili mwandamizi, Abdallah Chavulla walipinga vikali ombi hilo.

Wakili Chavulla alipinga ombi hilo akisema kisheria, hajaweza kuweka msingi wowote wa ufahamu wake juu ya tiketi hizo na wala hajaeleza nini kitamfanya azitambue tiketi hizo.

“Ni nyaraka ambazo si sisi wala Mahakama yako tukufu ambayo imeelezwa kama ni kweli hizo nyaraka ni za mabasi hayo? Kwa msingi huo tunaomba zisipokewe kama kielelezo,” alidai Wakili Chavulla.

Akijibu hoja hizo, wakili Safari alidai hoja hizo za upande wa mashtaka hazina msingi wa kisheria na ni potofu kwa kiwango cha juu na zenye lengo la kuipotosha Mahakama.

“Shahidi wetu (Mussa) ameshaeleza hapa kuwa tiketi hizi zina jina lake la Mussa Juma Mangu ambalo ni jina lake mwenyewe. Hakuna ubishi zilitolewa na mabasi hayo. Hili pingamizi halina msingi,” alidai.

Katika uamuzi wake, Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo, alitupilia mbali pingamizi hizo akisema shahidi ameweza kujenga msingi wa ushahidi wake na kielelezo kina uhusiano na kesi hiyo.

Baada ya kupokewa, mshitakiwa alipata fursa ya kuzisoma ambapo zilionyesha aliondoka Arusha Agosti 1 saa 12:00 asubuhi kwenda Singida na kutoka Singida saa 3:00 asubuhi kwenda Arusha.

Msuya anayemiliki vitega uchumi kadhaa, aliuawa kwa kupigwa risasi Agosti 7 mwaka jana saa 6:30 mchana eneo la Mijohoroni wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Kesi hiyo inaendelea leo