KKKT yaagiza makanisa kuombea mvua

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dk Fredrick Shoo

Muktasari:

Waraka huo uliosainiwa na mkuu wa kanisa hilo, Askofu Dk Fredrick Shoo, kwa niaba ya maaskofu wote, umesambazwa katika dayosisi na sharika zote za kanisa hilo na ulisomwa katika ibada zote za Jumapili.

Moshi. Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limesambaza waraka maalumu unaoelekeza makanisa yake yote nchini, kufanya maombi maalumu Jumapili ijayo kwa ajili ya kuomba mvua inyeshe.

Waraka huo uliosainiwa na mkuu wa kanisa hilo, Askofu Dk Fredrick Shoo, kwa niaba ya maaskofu wote, umesambazwa katika dayosisi na sharika zote za kanisa hilo na ulisomwa katika ibada zote za Jumapili.

Askofu Shoo alisema katika mkutano uliofanyika Arusha Januari 16 na 17 mwaka huu, kanisa lilitafakari hali ya ukame inayoendelea katika baadhi ya maeneo nchini.

“Ukame huu umetokana na kutokuwepo kwa mvua za vuli na za masika. Mamlaka ya hali ya Hewa ilishatoa tahadhari ya uhaba wa mvua katika msimu huu,” unasema waraka huo.