KKKT yajipa wiki moja kutoa tamko

Muktasari:

  • Hayo yalisemwa jana na Mchungaji Njama wakati akitoa taarifa ya tukio hilo kwa waumini katika ibada iliyofanyika jana asubuhi katika usharika huo uliopo Soweto.

Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), itatoa tamko kuhusu kukamatwa na kuhojiwa kwa mchungaji wake wa Usharika wa Karanga, Fred Njama Jumapili ijayo.

Hayo yalisemwa jana na Mchungaji Njama wakati akitoa taarifa ya tukio hilo kwa waumini katika ibada iliyofanyika jana asubuhi katika usharika huo uliopo Soweto.

Mbali ya kueleza hayo, mchungaji huyo aliwaeleza waumini wake tukio zima la kukamatwa kwake na kuhojiwa. Alisema Ijumaa iliyopita, aliitwa na kuhojiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Moshi kuhusiana na hotuba yake aliyoisoma katika mkutano mkuu wa 21 uliofanyika Machi 10.

Mchungaji Njama alidai kuwa baada ya kuhojiwa, wajumbe wa kamati hiyo walitaka wapelekwe walikochapishia vitabu vya mkutano huo. Aliwaeleza kuwa kamati hiyo ikiwa na polisi wenye silaha walifika kiwandani hapo na kuchukua kitabu kimoja.

“Kabla ya kwenda kuchukua vitabu ilitumika nguvu ya ziada. Walitaka kujua kilikochapishiwa na walipofika badala kwenda wachache waliingia wengi na wakachukua kitabu kimoja na kuja hapa kanisani,” alidai.

Hata hivyo hakufafanua kama polisi walichukua Laptop yake na Flush, lakini alisema baadaye walimchukua hadi polisi alipoandikisha maelezo hadi saa 3:30 usiku alipoachiwa kwa dhamana ya polisi.

Akifafanua kuhusu sakata hilo, Mchungaji Njama alisema, “Kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu, taarifa yetu ilipelekwa katika ofisi ya dayosisi na kuhakikiwa na baadaye ikarudishwa baada ya kuonekana ni sahihi,” alisema Mchungaji Njama.

“Baada ya mkutano ule nilipokea wito wa kuitwa na kamati ya ulinzi na usalama wilaya, ambapo nilitoa taarifa ofisi ya dayosisi na kupewa watu wawili nitakaoongozana nao akiwamo mwanasheria wa dayosisi yetu.

“Nilifika lakini wale nilioongozana nao hawakuruhusiwa kuingia. Kikao kile kiliongozwa na Mkuu wa Wilaya (Kippi Warioba) na baada ya mazungumzo marefu tulikubaliana kitabu kile kirudishwe dayosisi.

Warioba hakupatikana jana kwa simu kuzungumzia madai hayo na juzi alipotafutwa alimtaka mwandishi kwenda kuonana naye ana kwa ana lakini alipokwenda mchana alielezwa kwamba hajafika tangu asubuhi.

Mchungaji Njama alisema baada ya tukio hilo, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Dk Frederick Shoo ambaye pia ni mkuu wa KKKT, aliagiza Baraza Kuu la Dayosisi likutane kwa dharura hiyo jana na vitabu vyote vikusanywe na kurudishwa kwenye ofisi hizo.

“Askofu (Dk Shoo) ameagiza kukusanywa kwa vitabu vyote vya taarifa ya mkutano wetu mkuu wa 21 na atatoa tamko la Kanisa Jumapili ijayo hivyo tuwe watulivu na kuliombea hili,” alisema Mchungaji Njama.

Hata hivyo, alisema, “Kanisa lina sehemu yake katika nchi na kanisa halifundishwi nini liseme na nini lisiseme.”