Kabudi awasihi Watanzania Marekani wasaidie kukuza biashara

Muktasari:

Aulizwa swali la shambulio la Lissu

Manyara. Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi amewaomba Watanzania wanaoishi Marekani wasaidie kuimarisha biashara ili kukuza uchumi.

Kuonyesha uzito wa jukumu hilo, waziri aliwaambia Serikali ina wanategemea sana hasa kwa kuzingatia ujuzi, uzoefu na mchanganyiko wa maarifa waliyonayo katika kukuza biashara na uchumi wa Tanzania kwa kuzitumia vyema fursa zilizopo nje ya nchi.

“Serikali haitaki mtume misaada. Hatutaki muongeze kiasi cha remittances (fedha zinazotuma nyumbani) bali maarifa mliyonayo. Shirikianeni na wajasiriamali waliopo nyumbani kukuza biashara kati ya Tanzania na Marekani,” alisema Profesa Kabudi.

Waziri huyo aliwaeleza Watanzania hao kuwa mambo mengi yamebadilika nyumbani na mikakati iliyopo ni kukuza uchumi na mchango wa sekta binafsi unahitaji zaidi kufanikisha hilo.

Aliwaambia kwa kuishi kwao Marekani wanafahamu zaidi bidhaa za Tanzania ambazo zinaweza kupata soko la uhakika nchini humo.

“Vitunguu vingi vinavyoletwa na Kenya Marekani vinalimwa Karatu. Kuna vijana pale njia panda ya kwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wengine Kawe kama unaenda Hoteli ya Whitesands wanatengeneza samani nzuri sana. Ninyi mnafahamu mahitaji ya Marekani, shirikianeni nao kulitumia soko la Agoa,” alisema Kabudi.

Miongoni mwa mikakati ya kufanikisha ombi lake, waziri huyo aliwataka Watanzania hao kuanzisha biashara wakiwa Marekani ambazo zitasaidia kukuza ujasiriamali hapa nchini.

“Tanzania ina rasilimali nyingi, huenda mlikuwa hamjui, vinyago vilivyopo kwenye jingo la Umoja wa Mataifa vimetengenezwa Tanzania,” alisema.

JPM apiga simu

Akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika jijini Seattle juzi usiku, Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Willson Masilingi alisema Rais John Magufuli alikuwa anafuatilia matangazo yaliyokuwa yanarushwa moja kwa moja na Shirika la Utangazi Tanzania (TBC1) akiwa Chato mkoani Geita. 

"Wakati waziri anazungumza, Rais alinitumia sms na wakati naijibu akanipigia. Ameniambia yupo Chato anafuatilia mkutano tangu jana. Waliozungumza amewasikia, anawapongeza wote na atatekeleza, tumpigie makofi Rais," alisema Balozi Masilingi.

Uraia  

Profesa Kabudi alizungumzia suala la uraia wa nchi mbili ambao Watanzania hao walipendekeza mabadiliko ya Katiba yafanyike ili kuruhusu suala hilo jambo walilosema litasaidia kuchochea maendeleo.

Waziri alisema maoni mengi yaliyotolewa kwenye mabaraza ya maoni ya mabadiliko ya Katiba yalipinga suala hilo na kuwaeleza kuwa Serikali haina mpango huo kwa sasa.

“Wenzetu wanaoishi mipakani walikataa katakata uraia pacha kwa sababu ya usalama. Ukiacha hilo kuna suala la ardhi nalo ni changamoto ya nchi nyingi zinazotuzunguka. Kwenye ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda mpaka Tanga, licha ya kuwa na umbali mrefu zaidi sisi tumeshamaliza lakini Waganda bado wanavutana kuhusu fidia,” alibainisha Kabudi.

Jambo linalowezekana kwa sasa alisema ni kuandaa mpango wa kuwa na vitambulisho maalumu kwa Watanzania waliobadili uraia wao ili waweze kuingia nchini bila viza au watoto wao kuonekana wageni wakija Tanzania.

Waziri huyo alitumia fursa hiyo pia kutoa somo la uraia alisema upo wa aina tatu. Kwanza ni wa kuzaliwa halafu wa kuandikishwa na mwisho wa kurithi.

Raia wa kurithi ambaye ni mtoto aliyezaliwa nje ya Tanzania kwa wazazi wa Kitanzania, waziri alisema hawezi kugombea urais wa nchi.

"Nilikaa Ujerumani miaka mingi. Nina watoto wamezaliwa huko na huwa nawaambia wasahau kuhusu kugombea urais kwani Katiba haiwaruhusu. Inataka mtu aliyezaliwa Tanzania,” alisema.

Ikitokea wenye uraia wa kurithi wakazaa, Kabudi alisema mtoto hawi Mtanzania hivyo atapaswa kuomba kuwa uraia.

Lissu

Akijibu swali la mmoja wa Watanzania hao aliyetaka kujua uchunguzi wa shambulio la Tundu Lissu aliyepigwa risasi mchana kweupe na wahusika kutokamatwa hadi sasa umefika wapi, Kabudi alisema bado vyombo husika vinaendelea kutekeleza majukumu ya kuwasaka wahalifu husika.

Akijibu swali hilo, Profesa Kabudi alisema uchunguzi wa baadhi ya matukio ni mgumu hivyo kuhitaji muda mrefu zaidi kuukamilisha na hali hiyo si kwa Tanzania pekee.

 

"Hapa Marekani mlipo, Rais John F. Kennedy na ndugu yake walipigwa risasi lakini pamoja na teknolojia waliyonayo, hadi leo waliofanya uhalifu huo hawajakamatwa," alikumbusha. 

Aliwaeleza pia kuwa Lissu ni ndugu yake kwani alisoma darasa moja na kaka yake ambaye ni wakili maarufu jijini Arusha, Alute Mughway na watoto wake wanamwita Alute baba mkubwa. 

"Katika mapambano ya kiuchumi siyo kila jambo la kulitafutia majibu haraka," alitahadharisha. 

Wajinga wakiwa wengi

Waziri Kabudi aliwataka Watanzania hao kurudi nyumbani na kuzitumia fursa zilizopo kwani mambo mengi yamebadilika na Serikali inaweka mikakati ya kukuza uchumi.

Aliwataka kuja kushirikiana na ndugu na jamaa zao waliobaki lakini akawakumbusha kuwa makini na kutoleta ujuaji mwingi.

“Msije mkarudi nyumbani na kujifanya wajuaji sana, mkawaona wenyeji ni wajinga. Kumbukeni, wajinga wakiwa wengi wanakuwa werevu,” alisema waziri.