Mughwai kulijibu Bunge stahiki za Lissu

Muktasari:

Katibu wa Bunge, Kagaigai alimwandikia barua Mughwai Novemba 27,2017 akimtaka alieleze ni stahiki zipi ambazo ndugu yao anastahili apewe na Bunge.

Dar es Salaam. Alute Mughwai,kaka wa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, amesema anatarajia kujibu barua iliyoandikwa kwake na Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai ikihoji stahiki ambazo chombo hicho kinapaswa kumpatia ndugu yake.

Akizungumza na MCL Digital, Mughwai amesema ameipata barua ambayo ataijibu na baadaye atazungumza na waandishi wa habari.

“Nilikuwa Nairobi (Kenya) ndiyo nimerejea, nitaijibu barua hiyo na nitaiwasilisha kabla ya Alhamisi halafu ndani ya siku mbili hizi nitawaeleza kila kitu kuhusu suala hilo na maendeleo ya afya ya Lissu,” amesema.

MCL Digital ilipotaka kujua ni stahiki zipi ambazo Bunge linataka kujua kwamba ndizo anazotakiwa  kupewa Lissu, Mughwai alijibu, “Hizo ndizo danadana ila nitawajibu.”

Katibu wa Bunge, Kagaigai alimwandikia barua Mughwai Novemba 27,2017 akimtaka alieleze ni stahiki zipi ambazo ndugu yao anastahili apewe na Bunge.

Kagaigai alieleza kuhusu barua hiyo siku mbili baada ya Lissu kuhoji sababu za Bunge kutojihusisha na matibabu yake tofauti na sheria zinavyotaka.

Lissu anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alikopelekwa tangu Septemba 7,2017 aliposhambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana akiwa ndani ya gari kwenye makazi yake eneo la Area D mjini Dodoma.

Kauli ya Lissu ilikuwa mwendelezo wa ya awali iliyotolewa na Mughwai aliyesema alishaiandikia ofisi ya Bunge kutaka ilipie gharama za matibabu ya mbunge huyo.

Katika mahojiano na Mwananchi hospitalini jijini Nairobi, Lissu alisema alimweleza Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alipokwenda kumjulia hali kuwa, “Bunge liko wapi” kutokana na kutofanya juhudi za kwenda kumuona tangu alazwe.

Pia, alieleza kushangazwa na kitendo cha chombo hicho kutogharimia matibabu yake licha ya kuwa ni stahili yake kisheria iwe anatibiwa ndani au nje ya nchi.