Kama unataka ajira mvizie JPM

Rais John Magufuli

Muktasari:

Rais Mgufuli alitoa agizo la kuajiriwa askari hao kwa Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange baada ya kuridhika na namna walivyojituma na uamuzi wao kujitolea kushiriki mazoezi ya mwezi mmoja ili kujiweka katika hali ya ukakamavu.

Bagamoyo. Ule msemo wa kulala maskini na kuamka tajiri, wanaoweza kuulezea vizuri ni  mgambo 30 na askari waliopitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) 40, ambao bila kutegemea  wamehakikishiwa ajira kwenye Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Amiri Jeshi Mkuu, Rais John Magufuli.

Rais Mgufuli alitoa agizo la kuajiriwa askari hao kwa Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange baada ya kuridhika na namna walivyojituma na uamuzi wao kujitolea kushiriki mazoezi ya mwezi mmoja ili kujiweka katika hali ya ukakamavu.

Mazoezi hayo ambayo kwa kitaalamu yanaitwa ‘amphibious landing’ yalifanyika Kijiji cha Baatini wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani, ikiwa ni  sehemu  ya maadhimisho ya miaka 52 ya JWTZ.

Rais Magufuli aliyekuwa ameongozana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein walishuhudia mazoezi ya kijeshi ya kukomboa eneo lililotekwa na maadui kwa ukanda wa majini.