Kamanda wa trafiki abariki kauli ya Mambosasa

Muktasari:

  • Haukuishia kuunga mkono tu, Kamanda Muslim amesema askari wa usalama barabarani wanatakiwa kuangalia makosa hatarishi yanayoweza kusababisha kutokea kwa ajali na kuachana na yale yasiyokuwa ya msingi.

Kamanda wa Kikosi cha Polisi wa Usalama Barabarani nchini, Fortunatus Muslim ameunga mkono kauli ya kamanda wa jeshi hilo Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kuhusu utendaji kazi wa trafiki.

Haukuishia kuunga mkono tu, Kamanda Muslim amesema askari wa usalama barabarani wanatakiwa kuangalia makosa hatarishi yanayoweza kusababisha kutokea kwa ajali na kuachana na yale yasiyokuwa ya msingi.

Juzi, Kamanda Mambosasa aliwataka askari hususan wa usalama barabarani kutumia busara katika utendaji kazi wao ili kuondoa malalamiko ya uonevu na kuwakandamiza raia na kusisitiza kuwa Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya kulinda raia na mali zao na kusimamia sheria.

Akizungumza na Mwananchi jana, Kamanda Muslim alisema askari wote wa kikosi hicho wanaelekezwa kuzingatia makosa hatarishi kwa kuwa kazi kubwa ya kikosi hicho ni kuhakikisha sheria za barabarani zinazingatiwa ili kupunguza ajali zinazogharimu maisha ya watu.

Alisema kuna makosa ambayo hayana athari kulingana na mazingira husika hivyo askari hawana sababu ya kuyapa kipaumbele.

“Naungana kabisa na Mambosasa ila mimi nisitumie neno busara labda niseme askari wakamate makosa hatarishi, mnamkamata vipi dereva kwa kosa la taa mchana au wiper mbovu wakati wa jua kali? Hayo yote hayawezi kusababisha ajali kwa nyakati hizo. Hapo ndipo linapokuja suala na mazingira, wiper zinatakiwa kufanya kazi kipindi cha mvua.”

Kuhusu askari wa usalama barabarani kumsimamisha dereva na kuanza kutafuta kosa, Kamanda Muslim alisema ni muhimu kwa madereva kuzingatia sheria si muda wote wanasimamishwa kwa sababu ya makosa.

“Tatizo ni kwamba madereva wenyewe wameshajenga mtazamo hasi, sio kila wakati askari anapokusimamisha lazima uwe na kosa inawezekana anataka kukupa tahadhari huko unakoelekea sio kuzuri hivyo uongeze umakini.

“Ninachosisitiza madereva wafuate sheria, waache kulalamika. Wakizingatia sheria sidhani kama hao askari watakuwa wanawasimamisha ovyo kama wanavyodai,” alisema Kamanda Muslim.

Pia aliungana na Mambosasa kuwataka madereva wasikubali kutoa fedha kwa askari bila kupata risiti zinazotokana na mashine au fomu namba 101 ya polisi inayofahamika kama ‘notification’.

Kadhalika alisema askari wa pikipiki maarufu kama tigo wataendelea kufanya kazi yao ya kuzuia uhalifu unaohusisha makosa ya jinai na usalama barabarani na kusisitiza kuwa hawana mamlaka ya kutoza faini.

Ukusanyaji wa mapato

Kamanda Muslim alionyesha kukerwa na watu wanaohusisha tozo zinazotokana na makosa ya barabarani na ukusanyaji wa mapato.

Alisema kazi ya kukusanya mapato inafanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tofauti na tozo zinazokusanywa na kikosi hicho kutokana na uvunjifu wa sheria barabarani.

“Nashangaa wanaosema tunakusanya mapato kwani Jeshi la Polisi lina biashara gani? Sisi tunatoza tozo zinazotokana na makosa ya barabarani na lengo letu ni kuzuia ajali na kuhakikisha usalama unakuwa wa kutosha katika barabara zetu.

“Tozo hizo zipo kwa mujibu wa sheria na anayepaswa kulipa ni yule aliyevunja sheria na inasimama badala ya kifungo kwa hiyo watu wanapaswa kutambua askari wa usalama barabarani hawakusanyi mapato.”

Hali ya usalama barabarani

Kamanda hiyo alisema hali ya usalama barabarani nchini imeimarika na ajali zinaendelea kupungua kwa kiasi kikubwa.

Alisema hiyo inatokana na askari wa kikosi hicho kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa sheria.

“Nikitolea mfano wa leo (jana) yaani ndani ya saa 24, nchi nzima kuna ajali tatu pekee. Hii ni hatua kubwa na siku nyingine hakuna ajali kabisa hayo ni matokeo ya usimamizi wa sheria kazi inayofanywa vizuri kabisa na askari wa kikosi cha usalama barabarani.

“Usimamizi wa sheria umeongezwa maradufu kwenye maeneo ya kuvukia watembea kwa miguu, nimesisitiza lazima dereva asimame aangalie pande zote ndipo apite hata kama hakuna mtu anayevuka. Kwa magari yanayosafiri ukaguzi unafanyika kabla hayajatoka vituoni na madereva tunawapima ulevi, huko njiani askari nao wanajipanga vizuri.”

Kamanda Muslim alisema jitihada zote hizo zinafanyika kuhakikisha ajali zinapungua au kutokomezwa kabisa.

Alisema, “Hatuwezi kuvumilia watu wapoteze maisha sababu ya madereva wazembe, hatutafungua ‘tuition’ barabarani ya kutoa elimu. Kama unataka elimu acha gari lako nyumbani ukija nalo barabarani na ukavunja sheria neno ni moja tu “kamata” na watalipa faini na wale ambao watakuwa wagumu zaidi kuelewa neno lao ni “funga” hawa tutawafungia leseni zao.”