Kamati kuchunguza kifo cha mjamzito

Muktasari:

Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Adoh Mapunda alitoa uamuzi huo juzi akiuagiza uongozi wa hospitali hiyo kutoa maelezo ya sababu za kifo hicho kilichotokea Januari 21.

Musoma. Serikali imeazimia kuunda kamati maalumu kuchunguza kifo cha mjamzito, Mkami Mirumbe (39), kinachodaiwa kutokea baada ya kukosa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara mjini Musoma.

Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Adoh Mapunda alitoa uamuzi huo juzi akiuagiza uongozi wa hospitali hiyo kutoa maelezo ya sababu za kifo hicho kilichotokea Januari 21.

Mapunda alisema kamati hiyo itahusisha wataalamu wa kada mbalimbali pamoja na ndugu wa marehemu.

“Kuna madai ya kuwapo harufu ya rushwa katika tukio hili, tutachunguza yote hayo na kuchukua hatua stahiki bila uonevu wala upendeleo kwa atakayebainika kuhusika na kifo hicho,” alisema Mapunda.