Kamati ya Bunge yalia na bajeti ya afya

Muktasari:

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema fedha zilizoombwa na wizara hiyo mwaka 2018/19 ni Sh898.3 bilioni.


Dodoma. Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii imesema kiasi cha fedha kilichotolewa katika bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto mwaka 2017/18 hakiridhishi na ni kinyume na matarajio ya mpango wa bajeti.

Akiwasilisha maoni ya kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya mwaka 2018/19, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba amesema hadi kufikia Februari 2018 wizara hiyo ilikuwa imepokea kiasi cha Sh576.5 bilioni (sawa na asilimia 53) ya bajeti ya mwaka 2017/18 ya Sh1.07 trilioni iliyopitishwa na Bunge.

Amesema kati ya fedha hizo, Sh190.75 zilipokewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya wizara. 

Awali, akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo mwaka 2018/19 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema fedha zilizoombwa na wizara hiyo mwaka 2018/19 ni Sh898.3 bilioni.

Kulingana na kiasi cha fedha kilichotengwa mwaka 2018/19, tofauti ya bajeti ya 2017/18 na 2018/19 ni  Sh172.6 bilioni.

“Uchambuzi wa kamati umebaini kuwa katika matumizi mengineyo, wizara imepokea Sh59.3 bilioni (sawa na asilimia 92.6) ya Sh64 bilioni zilizoidhinishwa na Bunge,” amesema Serukamba na kuongeza: 

“Fedha za miradi ya maendeleo, wizara ilitengewa Sh785 bilioni na hadi kufikia Februari Sh385.77 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 49 zilipokewa na wizara ili kuweza kutekeleza miradi hiyo.”

Amesema kati ya fedha hizo za maendeleo, Sh336.3 bilioni zilikuwa ni kutoka vyanzo vya ndani na Sh449.5 bilioni ni kutoka vyanzo vya nje.

“Kamati imebaini kuwa kati ya fedha zilizopokewa, fedha kutoka vyanzo vya ndani  ni Sh64.7 bilioni sawa na asilimia 19 tu ya fedha zilizoidhinishwa. Fedha za nje ni Sh321 bilioni sawa na asilimia 71.4 zilipokelewa,” amesema.

Serukamba amesema hadi kufikia Februari 2018, wizara ilikuwa imepokea Sh15.46 bilioni (sawa na asilimia 44) ya kiasi cha fedha kilichoidhinishwa cha Sh35.30 bilioni za matumizi ya kawaida katika Idara ya Maendeleo ya Jamii.