Kamati ya Bunge yakesha na Korosho

Muktasari:

Miongoni mwa mabadiliko hayo ya Sheria ya Fedha ni kutaka fedha za ushuru wa korosho inayouzwa nje, ziende zote katika mfuko mkuu wa Serikali.


Dodoma. Baada ya suala la fedha za korosho kutikisa upitishaji Bajeti ya mwaka 2018/19, kazi sasa imehamia katika kupitisha mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya Fedha ambayo pia inahusu suala hilo.

Na dalili za mwanzo za ugumu wa suala hilo zimeonekana baada ya Bunge kuahirisha shughuli zake jana kutokana na kile kilichoelezwa kuwa kutokuwepo na makubaliano katika Kamati ya Bajeti kuhusu baadhi ya mambo, hasa suala la ushuru wa korosho inayouzwa nje.

Miongoni mwa mabadiliko hayo ya Sheria ya Fedha ni kutaka fedha za ushuru wa korosho inayouzwa nje, ziende zote katika mfuko mkuu wa Serikali, ambayo itaamua matumizi tofauti na utaratibu wa awali wa asilimia 65 ya fedha hizo kwenda Mfuko wa Korosho.

Naibu Spika, Dk Tulia Ackson aliahirisha shughuli za Bunge mapema jana akisema Kamati ya Bajeti iliyotakiwa kuwasilisha maoni kuhusu Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2018, kutokamilisha kazi.

“Kwa sababu tunaitarajia Kamati ya Bajeti kutuletea maoni hapa na haijakamilisha, hatutaendelea na ratiba. Hivyo naahirisha shughuli za Bunge hadi (leo) kesho saa tatu asubuhi,” alisema Dk Tulia.

Lakini habari ambazo Mwananchi imezipata zinasema kulikuwa na mvutano mkubwa miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Bajeti kiasi cha kushindwa kuafikiana na hivyo kutokamilisha kazi ya kuandaa maoni yao.

Mwananchi ilidokezwa kuwa kamati hiyo inayoongozwa na Hawa Ghasia ilikaa kikao juzi hadi saa 7:00 usiku wa kuamkia jana wakiwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.

Vyanzo vilivyozungumza na Mwananchi vimedokeza kuwa miongoni mwa mambo yaliyowafanya kukaa hadi muda huo na kuendelea na kikao jana ni suala la mabadiliko yanayohusu zao la korosho, masuala ya kodi ya michezo ya kubahatisha, sheria ya kufuta Tume ya Mipango, na tafsiri ya maneno ambayo hayapo kikatiba.

Wabunge, hasa kutoka mikoa ya Kusini ambayo inalima korosho kwa wingi, wanataka Serikali ipeleke Sh210 bilioni za ushuru wa mauzo ya korosho nje, zikiwemo Sh80 bilioni za msimu uliopita uliokuwa na mafanikio kwa wakulima za zao hilo.

Fedha hizo ni sawa na asilimia 65 ya fedha zote za mauzo zilizotakiwa ziende Mfuko wa Maendeleo ya Korosho kwa ajili ya kuboresha kilimo cha zao hilo, kama ununuzi wa pembejeo, ujenzi wa maghala, ununuzi wa michezo na shughuli nyingine.

Kutokana na hayo, baadhi ya wabunge wameahidi kukomaa kupinga mabadiliko ya sheria hiyo baada ya kushindwa kuzuia Bajeti ya Serikali kutokana na athari zake kikatiba.

“Wabunge wa CCM waliopiga kura ya ndiyo kwenye bajeti hawajakosea wala kugeuka kwani haikuwa kura ya uamuzi kuhusu korosho. Wakiunga mkono Muswada wa Sheria ya Fedha watakuwa wamegeuka wananchi wao,” alisema Zitto Kabwe, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii.

Zitto alisema kuahirishwa kwa muswada wa Sheria ya Fedha, kulitokana na Kamati ya Bajeti kutotoa idhini uingizwe bungeni.

Lakini akawashauri wabunge kuwa kura walizopiga juzi kupitisha bajeti ni tofauti na uamuzi kuhusu korosho uliomo kwenye muswada huo.

Ujumbe kama huo ulitumwa na mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye.

“Tukapitishe leo maji, barabara, afya, mishahara ya wafanyakazi nk. Hoja yetu ya korosho tukutane kwenye Finance Bill (muswada wa sheria ya Fedha) kesho na keshokutwa. Tutaendelea kuipinga, bado naamini haina masilahi kwa wakulima wa korosho,” ameandika Nape katika akaunti yake.

Suala hilo liliwagusa wakulima wa zao hilo ambao mapema wiki hii walitua Dodoma kwa ajili ya kutaka kuzungumza na wabunge.

Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Tandahimba (Tafa), Faraji Njapuka alisema wamekuwa wakikatwa Sh10 kwa kila kilo kwa ajili ya maendeleo ya zao hilo wakati wa Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza Korosho (CIDTF).

“Tunataka watueleze, hizi fedha zinapelekwa wapi? Halafu tunakatwa Sh90 kwa kila kilo kwa ajili ya vyama vya ushirika, lakini inarudishwa Sh60. Tatizo linakuja kwenye ukaguzi maana inaonekana tunarudishiwa yote,” alisema Njapuka.

Naye Hassan Managogo, kutoka Chama cha Wakulima Luwika wilayani Nanyumbu, alisema licha ya Serikali kupunguza idadi ya tozo kutoka 16 hadi tano, makato yameongezeka badala ya kupungua.

Alizitaja tozo zilizokuwapo awali kuwa ni ushuru wa magunia, wa wilaya, wa ushirika, wa chama cha msingi (Amcos), wa unyaufu, uzito, kupuliza dawa, usafirishaji, kikosi kazi, gharama za benki, maghala, kamba, sindano, kusafirisha fedha, kurudisha fedha na bima.

Alisema tozo zilizobaki ni ushuru wa wilaya, Amcos, ushirika, usafiri na mfuko wa maendeleo ya korosho, ambao alisema umeshafutwa.

“Wakati tozo zilikuwa 16 tulikuwa tunakatwa Sh246 kwa kilo, sasa zimefika tano, makato yamekuwa Sh275.75,” alisema Namagogo.

Mwenyekiti wa mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (Mviwata), Abdul Gea alisema wakulima wana haki ya kudai asilimia 65 ya ushuru huo.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wabangua Korosho, Tumpale Magelema alisema Vietnam ilichukua mbegu za korosho Tanzania, lakini imeendelea kwa viwanda vya ubanguaji na uzalishaji duniani.

Mwenyekiti wa chama cha ushirika cha Tunduru na Namtumbo, Said Naoda alisema Serikali inataka kuchukua fedha za korosho wakati sekta hiyo ikiwa kwenye hali mbaya.

Naye Hassan Shangazi kutoka ushirika wa Handeni mkoani Tanga alisema fedha za korosho zinachukuliwa wakati wao ndiyo wameanzisha juhudi za mashamba mapya ya korosho.

Watishia kwenda mahakamani

Wakati baadhi ya wabunge wakisubiri mjadala wa Muswada wa Sheria ya Fedha, kambi ya upinzani imesema Serikali isipolipa fedha za ushuru wa korosho, watakwenda mahakamani.

Pia, kambi hiyo inayoundwa na Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi ilisema inaunga mkono kauli za wabunge wa mikoa ya Kusini ya kuandaa maandamano ya kuishinikiza Serikali kutoa zaidi ya Sh200 bilioni za ushuru huo.

Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, aliyekuwa akizungumza kwa niaba ya wenzake, alisema amani ni zao la haki na haki inapotoweka, inaweza kusababisha machafuko.

“Sisi wabunge, tutaendelea kupigania haki ndani ya Bunge na kama itakosekana tutakwenda mahakamani,” alisema.

Nyongeza na Elias Msuya