Kamati ya Bunge yashauri ranchi za Taifa kurejeshwa serikalini

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa akiwasilisha bungeni maoni ya kamati hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mifugo  na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Imesema Tanzania ina jumla ya ranchi 13 zenye ukubwa wa hekta 627,856 katika mikoa 10


Dodoma. Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo ma Maji imeishauri Serikali kuzirejesha katika umiliki wake ranchi zote za Taifa walizopewa wawekezaji na kushindwa kuziendeleza.

Akisoma maoni ya kamati hiyo leo Mei 17, 2018 bungeni, Mwenyekiti wake, Mahmoud Mgimwa amesema ranchi za Taifa ni rasilimali muhimu na fursa ya kuchangia pato la Taifa na uchumi wa wafugaji.

Amesema Tanzania ina jumla ya ranchi 13 zenye ukubwa wa hekta 627,856 katika mikoa kumi.

“Uchambuzi uliofanywa na kamati umebaini hali ya uwekezaji uliopo katika Ranchi za Taifa haukidhi na hauendani na fursa ya ukubwa wa rasilimali zilizopo,” amesema Mgimwa.

Amesema kutokana na matumizi kidogo ya maeneo ya ranchi, wananchi waishio karibu na ranchi hizo wamekuwa wakivamia na kulisha mifugo yao na kusababisha migogoro isiyokuwa ya lazima.

“Ili kuondokana na changamoto hii kamati inashauri ranchi zote walizopewa wawekezaji na kushindwa kuziendeleza zirudishwe serikalini ili Serikali iweze kuziendeleza kwa kuziboresha zitumike kama maeneo ya malisho kwa wafugaji waishio pembezoni mwa ranchi hizo,” amesema Mgimwa.