Kamati yahoji Sh755.29 bilioni kutopelekwa mifuko maalumu

Muktasari:

Fedha hizo zinajumuisha Sh273.89 bilioni zilizokusanywa kama ushuru wa maendeeleo ya reli, lakini hazikupelekwa kwenye miradi iliyokusudiwa.

Dar es Salaam. Kamati ya Bajeti imehoji Sh755.29 bilioni ambazo Serikali ilikusanya lakini ikashindwa kuzipeleka kwenye mifuko maalumu iliyoanzishwa kwa ajili ya mikakati ya maji, umeme, reli na miradi ya barabara.

Fedha hizo zinajumuisha Sh273.89 bilioni zilizokusanywa kama ushuru wa maendeeleo ya reli, lakini hazikupelekwa kwenye miradi iliyokusudiwa.

Kamati hiyo imelitaka Bunge kuishauri Serikali kutoiingilia mifuko hiyo kwa kuwa kufanya hivyo kunaathiri ufanisi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hawa Ghasia alisema fedha za mifuko hiyo zina uzio wa kisheria (ring-fenced) na hazitakiwi kuwekwa katika mfuko mkuu wa Serikali.

Ghasia alisema hayo juzi alipokuwa akiwasilisha maoni ya kamati yake baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuwasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha.

Alisema uchambuzi walioufanya kwenye mfuko wa barabara (Road Fund) unaopata mapato yake kutokana na ushuru wa magari ya kigeni mpakani, tozo ya mafuta ya petroli, dizeli na faini ya magari yanayozidisha uzito, uliidhinishwa Sh917.548 bilioni mwaka 2017/18 lakini hadi Aprili, ni Sh628.637 bilioni sawa na asilimia 68.5 zilikuwa zimekusanywa na Wizara ya Fedha na Mipango.

Alisema kati ya fedha hizo, Sh604.489 bilioni ndizo zilipelekwa bodi hiyo, huku takwimu zikionyesha hadi Aprili, zaidi ya Sh24.148 bilioni zilikuwa hazijawasilishwa.

“Kamati inapendekeza Bunge lipewe taarifa ya makusanyo na utolewaji wa fedha hizo kwa Mei na Juni ili mfuko huo uweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu,” alishauri Ghasia.

Kuhusu Mfuko wa Umeme Vijijini (Rea), Ghasia alisema uliidhinishiwa Sh499.09 bilioni, lakini mpaka Machi Serikali ilikuwa imekusanya Sh446.911 bilioni.

Alisema taarifa ya Wizara ya Fedha na Mipango inaonyesha kiasi kilichopelekwa na kupokelewa Rea kilikuwa Sh251.311 bilioni zinazotokana na tozo ya mafuta tu. Aidha, Sh165.074 bilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo hazikuwasilishwa.

Kamati hiyo pia ilisikitishwa na kiasi kidogo kinachotolewa kutekeleza miradi ya maji.

Mfuko wa maendeleo ya maji unategemea tozo ya Sh50 katika mafuta ya taa, petroli na dizeli.

Mwaka huu mfuko ulitengewa Sh129.563 bilioni, lakini hadi Machi Serikali ilikuwa imekusanya Sh117.457 bilioni.