Wednesday, January 11, 2017

Kambi ya Lipumba yachukua ruzuku CUF

Mwenyekiti wa Chama Cha wananchi CUF, Profesa

Mwenyekiti wa Chama Cha wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi ebahemu@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kambi inayoongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba kwenye mgogoro unaoendelea ndani ya CUF imechukua Sh369.4 milioni kutoka serikalini ikiwa ni mgawo wa ruzuku ya chama hicho.

Kambi nyingine katika mgogoro huo inaongozwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro amesema wanachama wanaomuunga mkono Profesa Lipumba walichukua fedha hizo kupitia akaunti ya CUF wilaya ya Temeke, kisha wakazihamishia katika akaunti binafsi tofauti.

“Kilichofanyika ni kama leo hii ruzuku ya CCM itoroshwe na kuwekwa kwenye akaunti ya chama hicho ngazi ya wilaya huko Kahama bila idhini ya katibu mkuu wake Abdulrahman Kinana,” amesema.

Upande wa Profesa Lipumba kupitia kwa mkurugenzi wa mawasiliano wa CUF aliyeteuliwa na Profesa Lipumba, Abdul Kambaya umethibitisha kuchukua fedha hizo.

Amesema baada ya kukaa bila ya pesa ya ruzuku, chama kiliamua kumwandika barua Msajili ili arejeshe ruzuku aliyoizuia kwa chama hicho.

“Fedha tulichukua. Lakini kwa mazingira yaliyopo, kama tungemshirikisha katibu mkuu huenda fedha zingezuiwa. Chama kinahitaji fedha kwa ajili ya uchaguzi huu mdogo wa madiwani ambao takriban Sh140 milioni zitatumika,” amesema.Kaimu mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha Wizara ya Fedha, Benny Mwaipaja amesema Wizara ya Fedha imetoa ruzuku ya Sh7.1 bilioni kwa vyama vya siasa kuanzia Julai hadi Novemba 2016 na kiutaratibu fedha hizo zilipelekwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye ndiye mwenye jukumu la kuzigawa kwa vyama husika.

 

 

-->