Kampeni ya Makonda yakosolewa bungeni Dodoma

DAKIKA 20 ZA WABUNGE NANE WAKIKOSOA KAMPENI YA WANAWAKE WALIOTELEKEZEWA WATOTO

Muktasari:

  • Jana, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alisema kampeni hiyo ya kuwasaidia wanawake waliotelekezwa na waume zao wakiwa na watoto ilipaswa kufanyika kwa faragha.

Dodoma. Kampeni iliyofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda iliyolenga kuwasikiliza wanawake wanaodai kutelekezwa na wanaume waliozaa nao, imekosolewa ndani ya Bunge.

Jana, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alisema kampeni hiyo ya kuwasaidia wanawake waliotelekezwa na waume zao wakiwa na watoto ilipaswa kufanyika kwa faragha.

Profesa Kabudi alisema hayo wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha bajeti ya wizara hiyo baada ya Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga kuhoji uhalali wa kampeni hiyo.

Waziri Kabudi alisema shughuli hiyo inaweza kuleta hali ya sintofahamu akibainisha inapaswa kufanyika kwa faragha na si kama inavyofanyika sasa.

Wakati waziri akisema hayo, Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma alisema kampeni ya Makonda ni ishara ya kukosa kazi ya kufanya.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema kampeni hiyo ni sahihi, lakini kasoro yake ni kutokuwa na faragha.

Akizungumzia kampeni hiyo hivi karibuni, Makonda alisema kwa siku tano wanawake 4,400 walisikilizwa na familia 295 zilifikia makubaliano ya kulea watoto kwa kushirikiana, huku wanaume 29 wakipimwa vipimo vya vinasaba (DNA) kuthibitisha kama kweli ni wazazi wa watoto wanaodaiwa kuwatelekeza.

Alisema kati ya malalamiko yaliyopokewa, 117 yaliwahusu wanasiasa, viongozi wa dini na watu wenye majina makubwa kwenye jamii na kwamba kampeni hiyo lengo lake ni kulinda haki ya mtoto.

Kampeni hiyo iliyoanza Aprili 9 ilikuwa ya siku mbili lakini kutokana na idadi kubwa ya watu, muda umeongezwa hadi Aprili 20.