Kampeni zaanza kwa pingamizi

SALUM MWALIMU AREJESHA FOMU ZA UBUNGE KINONDONI

Muktasari:

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Jeshi la Polisi wametia ‘mguu’ katika uchaguzi huo, wakiwahakikishia wananchi kuwa watafuata sheria na kanunu na kwamba amani itatamalaki.

Dar es Salaam. Wakati kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Kinondoni na Siha, zikianza kwa vitimbi, mgombea wa CCM, Maulid Mtulia amewekewa pingamizi lenye vipengele vitano.

Pia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Jeshi la Polisi wametia ‘mguu’ katika uchaguzi huo, wakiwahakikishia wananchi kuwa watafuata sheria na kanunu na kwamba amani itatamalaki.

Uchaguzi huo utakaoshirikisha vyama 12, utafanyika Februari 17 huku ukitarajiwa kuwa na mpambano mkali baina ya CCM na Chadema inayoungwa mkono na vyama vitano vya Ukawa ambavyo NLD, NCCR-Mageuzi, CUF ya upande wa Maalim Seif Sharif Hamad na Chaumma iliyojiunga hivi karibuni.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya waliokuwa wabunge, Godwin Mollel (Siha, Chadema) na Maulid Mtulia (Kinondoni, CUF) kujivua uanachama kwa maelezo kuwa wanamuunga mkono Rais John Magufuli na baadaye kujiunga na CCM.

Chama hicho tawala kimewapitisha wawili hao kutetea majimbo hayo bila ya kuendesha mchakato wa ndani.

Kwa staili kama hiyo, Chadema imemsimamisha Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu katika jimbo la Kinondoni na Elvis Mosi (Siha).

Tayari CCM katika jimbo la Siha na CUF upande wa mwenyekiti anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba wamezindua kampeni jana.

Chadema yaweka pingamizi

Wagombea walirejesha fomu juzi katika ofisi ya jimbo la iliyopo Magomeni.

Lakini saa chache kabla ya kuanza kampeni, Mwalimu aliwasilisha pingamizi dhidi ya mgombea wa CCM, akiwa na hoja tano, ikiwemo ya kutofanya mrejesho wa gharama za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Wakili wake, Frederick  Kihwelo aliliambia Mwananchi kuwa kwanza, Mtulia  hajafanya mrejesho wa gharama za uchaguzi wa mwaka 2015, alipogombea kwa tiketi ya CUF.

“Jambo hili hufanywa na mtu yeyote aliyegombea nafasi ya udiwani, ubunge na urais na haijalishi kama alishinda au kushindwa,” alisema Kihwelo.

“Unapaswa kuandaa mchanganuo wa gharama zako za uchaguzi na kuzipeleka ofisi ya NEC.”

Alisema hoja ya pili ni Mtulia kushindwa kukidhi matakwa ya kisheria kwa kutojaza kwa usahihi fomu zake, kwa madai kuwa zimepigwa muhuri wa katibu wa CCM badala ya muhuri wa chama hicho tawala.

“Muhuli ulipigwa katika fomu yake unasomeka wa katibu wa chama badala ya muhuri wa chama. Hii inaonyesha chama hakijamthibitisha kugombea. Jambo hili liliwasumbua sana Chadema mwaka 2014 kwa baadhi ya wagombea wao kuenguliwa, ” alisema Kihwelo.

Alisema hoja ya mwisho ni Mtulia kujaza fomu akieleza kuwa anajishughulisha na kilimo cha mbogamboga, jambo ambalo Kihwelo amesema si kweli.

“Hiki kilimo cha mbogamboga amekianza lini kwa sababu tunajua alikuwa mbunge. Tunamtaka athibitishe hili,” alisema.

Mwananchi lilipomtafuta Mtulia kujibu hoja hizo alijibu kwa kujiamini kuwa “hili jambo ni jepesi sana na nimeandika ninachokijua na hakuna pingamizi hapo”.

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa Kinondoni, Latifa Almasi alisema wamepokea mapingamizi lakini haweka wazi idadi yake, na kubainisha kuwa leo msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, Aron Kagurumjuli, atayatolea ufafanuzi

NEC wazungumzia kasoro

Vyama sita vya upinzani vilijitoa katika uchaguzi mdogo wa madiwani katikakata 43, vikidai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria na kanuni baada ya mawakala wao kuzuiwa kuingia vituoni, wagombea kukamatwa, wakuu wa wilaya kuingilia kati na viongozi kukamatwa.

Baadaye vikasusia uchaguzi katika majimbo matatu vikishinikiza kukutana na NEC kwa ajili ya kujadili kasoro za uchaguzi wa madiwani, lakini Tume hiyo haikukutana navyo.

Hata hivyo, vyama hivyo vimesema baada ya uchaguzi wa majimbo matatu kutokuwa na vurugu na ukiukwaji wa sheria na kanuni, vimeamua kuingia katika mpambano wa majimbo hayo mawili.

“Vyama ndivyo havitaki kufuata sheria,” alisema mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima alipoulizwa kuhusu malalamiko ya vyama hivyo.

Kuhusu mawakala kuondolewa vituoni, Kailima alisema kwa mujibu wa kifungu cha 58 cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, wakala anatakiwa kuwa na barua utambulisho kutoka kwenye chama cha siasa, kiapo cha uaminifu na barua ya utambulisho kutoka NEC.

Hata hivyo, alisisitiza kwamba masharti hayo ya kisheria hayafuatwi kikamilifu na vyama vya siasa na pale wanapotakiwa kufuata taratibu wanalalamikia Tume, wakidai kwamba wanafukuzwa kwenye vituo.

“Hakuna wakala yoyote mwenye sifa ambaye anafukuzwa kituoni. Hakuna kitambulisho chochote kinachotakiwa wakala akiwa na mambo hayo matatu,” alisema Kailima.

Alisema barua ya utambulisho wa wakala kutoka Tume inatakiwa kuwa na jina la wakala, anuani na kituo atakachosimamia.

Kuhusu kuchelewa kuapishwa kwa mawakala, Kailima alisema: “Kisheria mawakala wanatakiwa kula kiapo siku saba kabla ya kupiga kura, lakini vyama vimekuwa vinachelewa kuleta majina ya mawakala wao. Ni huruma ya Tume kuwaapisha, muda ukipita hawatakiwi kuapishwa kabisa.”

Kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo, Kailima alisema maandalizi yamekamilika na uteuzi wa wagombea kwenye majimbo ya Kinondoni na Siha na baadhi ya kata umefanyika huku uteuzi mwingine wa wagombea ngazi ya udiwani ukitarajiwa kutangazwa Januari 24.

Polisi waahidi amani

Askari wa Jeshi la Polisi walituhumiwa kuvuruga uchaguzi wa madiwani kwa kukamata mawakala, wagombea na viongozi wa vyama vya upinzani

“Tumejiandaa kikamilifu kuhakikisha kampeni za uchaguzi mdogo zinafanyika kwa amani na usalama,” alisema kamanda wa polisi mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo.

Murilo alisema watakabiliana na wafuasi wa vyama vya siasa ambao hakuwataja, akisema wamejipanga kuvuruga uchaguzi huo kwa kufanya vurugu siku ya kupiga kura.

Alisema jeshi hilo litakuwa macho wakati wote kuhakikisha amani inakuwapo.

“Ni wajibu wetu kulinda usalama wa raia na mali zao. Tumekuwa tukifanya hivyo kabla na kwenye kipindi cha kampeni za uchaguzi tutakuwa macho kweli. Ninawahakikishia wananchi kwamba hali itakuwa shwari,” alisema Kamanda Murilo.

Mpambano katika uchaguzi huo unachangiwa na vitu kadhaa, hasa kutokana na ukweli kuwa Chadema na vyama vingine rafiki vitakuwa vikipambana na mtu viliyempigania ashinde ubunge mwaka 2015 chini ya mwamvuli wa Ukawa.

“Katika uchaguzi huu kutawaka. Hatutakubali kuchezewa kama ule uchaguzi wa Kata 43, tunataka haki itendeke la sivyo hakitaeleweka,” alisema mwenyekiti wa Chadema alipoongea na Mwananchi.

Wakati hayo yakiendelea, vyama vya NCCR Mageuzi, Chaumma na NLD vimetangaza kuunga mkono wagombea wa Chadema kwenye uchaguzi wa majimbo hayo.

Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe alisema watamuunga mkono mgombea wa Ukawa kwa sababu jimbo hilo lilikuwa la Ukawa kabla ya mbunge wake kutimkia CCM.

Rungwe alisema walijitoa kwenye uchaguzi mdogo uliopita kwa sababu mazingira yake hayakuwa ya haki na waliiandikia barua NEC kulalamikia uchaguzi huo hasa kutumika kwa vyombo vya dola kuwakandamiza wapinzani.

“Tulipopeleka malalamiko yetu Tume, walituambia kwamba wamewaandikia barua wakuu wa mikoa na wilaya kutoingilia chaguzi kwenye maeneo yao,” alisema Rungwe.

“Kwa hiyo tunaamini uchaguzi huu utakuwa na fair (wa haki) na mgombea tunayemuunga mkono atashinda,” alisema Rungwe.

Kauli kama hiyo ilitolewa pia na viongozi wa Juju Danda (NCCR-Mageuzi) na Tozi Matwanga (NLD).

ACT-Wazalendo yajitenga

Lakini ACT Wazalendo, ambayo pia ilisusia uchaguzi katika majimbo matatu, imeeleza kumeshangazwa na hatua ya Chadema na vyama vingine kuingia kwenye uchaguzi kwa maelezo kuwa mazingira bado hayajakuwa sawasawa.

Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo (Bara), Msafiri Mtemelwa alisema bado kuna umuhimu kwa vyama vya upinzani kuikabili NEC na vyombo vya dola kwa pamoja.

“Hatutasimamisha wagombea ubunge kwenye majimbo ya Siha na Kinondoni,” alisema.

Mtemelwa alisema sababu zilizowafanya wasusie uchaguzi wa Januari 13, 2018 bado hazijafanyiwa kazi na NEC na Jeshi la Polisi.