Kampuni ya Trend Solar kutoa umeme wa jua kwa mkopo

Balozi wa Uingereza nchi Tanzania, Sarah Crooke mwenye nguo nyeupe akiwa ameshika boksi lenye vifaa vinavyotolewa na Solartrend kwa wateja wake, kushoto kwake ni Mkuu wa masoko wa Startimes, David Malisa

Muktasari:

Kampuni hiyo iliyoanza kutoa huduma mwaka 2017 imelenga kuwaleta watu wa vijijini katika ulimwengu wa kidigitali.

Dar es Salaam. Kampuni ya Trend Solar inayotoa huduma ya umeme wa kulipia usiotegemea gridi imezindua uuzaji wa umeme wa jua nchini utakaosaidia wanaoishi vijijini kuondokana na matumizi ya mishumaa na vibatari.

Kampuni hiyo iliyoanza kutoa huduma mwaka 2017 imelenga kuwaleta watu wa vijijini katika ulimwengu wa kidigitali.

Akizungumza leo Julai 5  wakati wa uzinduzi wa programu hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Trend Solar, Irfan Mizra amesema katika kuzingatia vipato vya watanzania wateja wanapewa nafasi ya kulipia kidogo kidogo hadi watakapokamilisha malipo.

"Mteja anao uhuru wa kulipa hadi kwa muda wa miezi 18, wakati anaanza atalipia Sh139, 999 na kupewa huduma zote na ataendelea kulipia Sh17, 999 kila wiki ndani wiki ya 78," amesema Mizra.

Amesema mteja anaponunua mashine za umeme wa jua, hupewa luninga ya kisasa ya inchi 24 ya kampuni ya Star Times, simu ya smati 4g ya kampuni hiyo na chaja yake, tochi ya kuchaji, betri ya smati sola, taa nne aina ya Led na dishi la Star Times.

Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Sarah Cooke amesema watanzania wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo ili kupata maendeleo.

"Kwa wale waishio vijijini itakuwa ni nafasi kwao kuondokana na matumizi ya vibatari yanayoweza kuwaletea madhara kiafya huku wakifurahia huduma hiyo kwa  kulipia kidogo kidogo," amesema Cooke.