Kampuni 12 tu kati ya 140 zinaongozwa na wanawake nchini

Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba

Muktasari:

  • Taarifa zilizokusanywa na gazeti la The Citizen zimebaini kuwa ni kampuni 12 tu kati ya 140 nchini, ndizo zinazoongozwa na wakurugenzi wanawake.

Dar es Salaam. Licha ya juhudi kubwa kufanyika kuleta usawa wa kijinsia, taarifa zinaonyesha kuwa bado kuna safari ndefu kuziba pengo hilo hasa kwenye nafasi za uongozi katika taasisi na mashirika makubwa nchini.

Taarifa zilizokusanywa na gazeti la The Citizen zimebaini kuwa ni kampuni 12 tu kati ya 140 nchini, ndizo zinazoongozwa na wakurugenzi wanawake.

Gazeti hilo limefanya uchambuzi wa kampuni kubwa 140 na kuangalia zile zinazoongozwa na wanawake na kubaini kuwa wanawake wakurugenzi wapo 12 tu.

Hata hivyo hali hiyo ni tofauti kidunia, kwani idadi ya wakurugenzi wanawake inaongezeka ambapo mpaka mwaka 2016, karibu asilimia 16 ya nafasi katika kampuni kubwa zilikuwa zikiongozwa na wakurugenzi wanawake. Taarifa hizo zimekusanywa wakati dunia leo ikiadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, ambayo hufanyika Machi 8, kila mwaka.

Mwenyekiti wa maofisa watendaji wakuu wa Kampuni Tanzania (CEOrt), Ali Mufuruki alisema juhudi za dhati na za pamoja zinahitajika katika taasisi za umma na za Serikali kuhakikisha hakuna pengo wakati mila, dini, na tamaduni zikiendelea kuchangia kutokuwepo kwa usawa katika masuala ya jinsia.

“Usawa wa kijinsia ni mada pana, lakini ukweli hauweki wazi. Nchi inahitaji mabadiliko makubwa kuhakikisha wanawake wanapewa hadhi sawa na wanaume,” alisema Mufuruki.

Wakati huohuo, Baraza la Dunia la Uchumi (WEF) lilifanya utafiti uliochapishwa Novemba 2017, na kubaini kuwa kuna tofauti kubwa kati ya wanawake na wanaume katika maeneo mengi hasa ya kiuchumi na kutokana na changamoto hizo, itachukua miaka 217 kuliondoa pengo hilo.

Siku ya mwanamke

Akizungumzia siku ya wanawake duniani jana, mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema vitendo vya ukatili bado vinaendelea kuripotiwa na wanawake wamekuwa wahanga wakubwa wa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Dk Kijo-Bisimba alisema kuna haja ya kuwa na mpango maalumu wa kutoa elimu kwa jamii ili iondokane na matukio ambayo yanaripotiwa kila siku.

Alisisitiza kuwa Serikali kupitia jeshi la polisi lichukue hatua za haraka dhidi ya matukio yote yanayoripotiwa. “Siku kama hii tunajikumbusha kuhusu haki za wanawake na kwamba ukatili haufai. Wanawake wana umuhimu mkubwa kwenye jamii zao, lazima waheshimiwe na kulindwa,” alisema mkurugenzi huyo.

Akiwa na mtazamo kama huo, mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Edda Sanga alisema kuna haja ya kuwa na mjadala wa kitaifa juu ya haki za wanawake ili Taifa liwe na msimamo wa pamoja wa namna ya kumlinda mwanawake. Alisema mwafaka huo wa kitaifa utalifanya Taifa kuwa pamoja na kila mmoja kutimiza wajibu wake katika ulinzi wa haki za wanawake dhidi ya vitendo vya ukatili.

“Tunapenda kuona Serikali inakuwa na utashi mkubwa, kwa sasa utashi ni mdogo sana. Tunapenda kuona wanawake wengi wanateuliwa kwenye nafasi za uongozi katika idara na taasisi mbalimbali za serikali,” alisema Sanga.

Mwanasheria na rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), Felix Kibodya alisema uwiano wa hamsini kwa hamsini haujafikiwa kwa sababu jamii nyingi hazitaki kumtambua mwanamke na kwamba hawana uwezo wa kuwaongoza kuanzia ngazi ya familia mpaka taifa.

Alisisitiza kwamba jamii izidi kusomesha watoto wa kike ili wajitambue na kudai haki zao pale zinapokiukwa. Alisema Serikali inaweza kuongeza idadi ya wanawake kwenye nafasi za uteuzi na kuwapa nafasi kwenye majimbo badala ya kupewa nafasi za ubunge wa viti maalumu.