Kampuni iliyozua utata NSSF yatoa msaada wa ekari 1,500

Mkurugenzi Mkuu wa Azimio Housing Estate, Mohamed Ikbal (katikati) akimuonyesha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (wa tatu kushoto) eneo la ekari 1,500 alizokabidhi kwa serikali kwa ajili ya ujenzi wa viwanda katika eneo la Lingato Kisarawe II Kigamboni. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhiwa ekari hizo na Mkurugenzi wa Azimio Housing Estate, Mohamed Ikbal jana, mkuu wa mkoa aliwataka watu walio safi na mali zao kutoa maeneo au mchango wowote kwa ajili ya maendeleo ya viwanda vidogovidogo jijini hapa na wasifanye hivyo kutaka kujificha.

Dar es Salaam. Kampuni ya Azimio Housing Estate iliyoshirikiana na Shirika la Hifadhi la Taifa la Jamii (NSSF) katika miradi tata ya ujenzi, imemkabidhi ekari 1,500 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa ajili ya viwanda vidogovidogo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhiwa ekari hizo na Mkurugenzi wa Azimio Housing Estate, Mohamed Ikbal jana, mkuu wa mkoa aliwataka watu walio safi na mali zao kutoa maeneo au mchango wowote kwa ajili ya maendeleo ya viwanda vidogovidogo jijini hapa na wasifanye hivyo kutaka kujificha.

“Kama kuna mtu ana eneo au mchango wowote anakaribishwa, lakini changia kama mikono yako ni misafi kwanza siyo unachangia ukijua mikono yako ni michafu kama hulipi kodi, hutendi haki unategemea utajificha mimi nitakushughulikia,” alisema Makonda.

Makonda alisema eneo alilokabidhiwa la Lingati lililopo Kisarawe II, Wilaya ya Kigamboni litagawanywa sehemu tatu kwa ajili ya ufugaji wa ng’ombe wa kisasa, kilimo na shughuli za usindikaji wa bidhaa mbalimbali.

Ikbal alisema anaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli kwenye suala la viwanda hivyo kwa hiyari yake, ametoa ekari hizo. “Mkuu wa mkoa aliniomba niunge mkono mambo ya viwanda nimekubali kutoa ardhi kuunga mkono jitihada za Rais,” alisema.

Utata NSSF na Azimio

Kumbukumbu zilizopo Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na NSSF, zinaonyesha kuwa Azimio ilishirikiana na mfuko huo kujenga mji wa kisasa Kigamboni maarufu kama Dege Eco Village kwa Dola za Marekani 655 milioni (Sh1.254 trilioni) na ambao ulikwama wa mji wa Arumeru, Arusha wa thamani ya dola 3.34 bilioni (Sh7.2 trilioni).

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara aliiambia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) mwaka jana kuwa miradi ya Dege Eco Village na Arumeru iligubikwa na utata.

“Jumla ya gharama za mradi (Kigamboni) ni Dola za Marekani 653.44 milioni na utaratibu wa uchangiaji mtaji ni kuwa NSSF itatoa fedha zenye thamani ya asilimia 45 ya gharama za mradi na Azimio itatoa fedha zenye thamani ya asilimia 35 ya gharama za mradi pamoja na ardhi ambayo itathaminishwa kuwa asilimia 20 ya gharama za mradi,” alisema Profesa Kahyarara.

Katika taarifa hiyo, NSSF ilisema hadi mradi wa Kigamboni unasimama Februari 2016 shirika lilikuwa limetoa Dola 129 milioni sawa na Sh270 bilioni wakati Azimio ilikuwa imetoa dola 5.5 milioni na ekari 300 tu.

Pia, Profesa alisema mkataba wa ujenzi ulioonyesha kuwa uwekezaji kamili ungekuwa wa ekari 20,000 ambazo zingetolewa na Azimio lakini uhalisia baada ya kufanya tathmini zilipatikana ekari 3,503 tu.

Alisema tatizo jingine ni kwamba thamani ya ekari moja ilikubaliwa kwa Sh800 milioni wakati uhalisia baada ya tathmini thamani ya ekari moja ni Sh25 milioni na kwamba baada ya kugundua udanganyifu huo walianza kufanya uchunguzi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na hatua mbalimbali zilichukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha kazi waliohusika na madudu hayo.

Maoni ya wabunge

Akizungumzia kitendo cha mfanyabiashara huyo kumpa Makonda shamba hilo Mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea alisema ujenzi wa viwanda ni mzuri kwa manufaa ya wananchi lakini muhimu kumchunguza anayetoa.

Mbunge wa Mkuranga (CCM), Abdallah Ulega alisema jambo hilo ni la kiungwana na linatakiwa kuigwa kwa watu mbalimbali kuipa nguvu Serikali kujenga viwanda na wananchi kunufaika.

“Papai si haramu, ila kinachotokana na papai ndicho haramu ambayo ni pombe ya gongo. Sasa kama mtu katoa ardhi yake bure tupambane kupata viwanda maana ajira hakuna. Tupate Sido kubwa na siyo kuwaza mtu aliyetoa ardhi hiyo,” alisema Ulega.

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema mfanyabiashara huyo anatumia mwanya huo kujisafisha na hakupaswa kumpa Makonda badala yake Mkurugenzi na Meya wa Kigamboni ambao ndiyo watendaji walitakiwa kupokea.