Kampuni upimaji madini nchini yapewa cheti ya ubora

Muktasari:

Profesa Manya ambaye pia ni kamishna wa madini amesema  hayo alipokuwa akikabidhi cheti cha ubora wa kimataifa cha upimaji madini (ISO) kwa kampuni hiyo ya upimaji madini.

 


Dar es Salaam.  Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini Tanzania, Profesa Shukrani Manya ameitaka kampuni ya upimaji madini nchini, Nesch Mintech Private LTD kusimamia ubora katika upimaji ili kuwaepushia hasara wachimbaji.

Profesa Manya ambaye pia ni kamishna wa madini amesema  hayo alipokuwa akikabidhi cheti cha ubora wa kimataifa cha upimaji madini (ISO) kwa kampuni hiyo ya upimaji madini.

Amesema licha ya kampuni hiyo kuwa ya kwanza Afrika Mashariki kupata cheti hicho cha ubora, inapaswa kufanya kazi kwa uadilifu bila kupindisha mambo.

Amefafanua kuwa iwapo itafanya kiujanja ujanja itasababisha hasara kwa wachimbaji.

“Cheti hiki kitawapa uaminifu kwa wateja wao ambao ni wachimbaji wakubwa na wadogo, hivyo wasibweteke kwa sababu wamekipata, bali wafanye kazi kwa bidii kuhakikisha anabaki na ubora ule ule,”amesema.

“Kwa sababu kinadumu kwa miaka mitano, nawaomba Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika inayojishughulisha na kukagua na kutoa vyeti vya huduma za kimataifa (Sadcas) ambao ndiyo wanatoa cheti hiki kuwakagua mara kwa mara na wakiona wanafanya ndivyo sivyo wasisite kuwanyang’anya, ”amesema Profesa Manya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo , Happiness Nesvinga amesema watahakikisha wanasimamia yale yote yaliyosaidia kupata cheti hicho ikiwamo kuzingatia ubora.

Amesema anajua thamani ya kuaminiwa, iwapo watafanya tofauti wataondoa uaminifu na hatimaye kulitia doa Taifa kwa sababu wateja wao ni wa ndani na wa nje ya nchi.