Kampuni za TRL, Rahco kuvunjwa

Muktasari:

Shirika hilo litaundwa baada ya kuvunjwa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (Rahco).

Dodoma. Bunge limepitisha Muswada wa Sheria ya Reli ya mwaka 2017 ambayo itaanzisha shirika jipya la reli.

Shirika hilo litaundwa baada ya kuvunjwa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (Rahco).

Muswada huo uliopitishwa jana bungeni uliwasilishwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.

Akiwasilisha muswada huo, Profesa Mbarawa alisema shirika jipya litajulikana kwa jina la Shirika la Reli Tanzania (TRC), litakalokuwa na jukumu ya kusimamia, kuendeleza miundombinu ya reli na kutoa huduma ya usafiri.

Alisema watumishi waliokuwa chini ya TRL ni 1,900 na 38 wa Rahco.

Akiwasilisha maoni ya kamati, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Moshi Kakoso alisema wanaishauri Serikali kuweka utaratibu kwa mwananchi kupata haki zao yanapotokea matatizo ya kufutwa na kuchelewa kwa safari.

Alishauri Serikali kuweka utaratibu wa wazi na wa haki utakaotumika kuhamisha wafanyakazi kwenda kwenye shirika jipya au wengine kwenda ofisi zingine za Serikali.

Pia, kamati ilishauri bomoabomoa kwenye maeneo ya Shirika la Reli iendelee, isipokuwa wananchi walipwe fidia.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, pia ilishauri muda wa kuwarejeshea nauli abiria baada ya treni kuchelewa, uwe saa sita badala ya saa 24 ili kuwafanya watendaji wa shirika kuwajibika.

Akisoma maoni kwa niaba ya msemaji wa kambi hiyo, Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Jaffar Michael alisema kama Serikali itaona ni vyema muda ukabaki uleule, basi angalau kuwe na jukumu la shirika kuwapa abiria waliocheleweshwa chakula na malazi ili kuwapunguzia usumbufu.

Kuhusu faini kwa abiria, Michael alisema wanashangazwa na matakwa ya kifungu cha 47(2) kumtoza abiria asilimia 100 ya nauli pale anapopanda bila kuwa na tiketi.

“Ni ukweli usiopingika kuwa abiria wengi wanatoka maeneo ya mbali na njia ya reli, hivyo wanaweza kujikuta hawajakata tiketi ya safari au mara kadhaa ofisi za kutolea tiketi huwa zinakuwa na foleni na pengine abiria huwa na dharura,” alisema .

Alishauri anayepanda treni bila kuwa na tiketi angalau atozwe faini ya asilimia 50 ya nauli iliyotakiwa kutozwa.

Wabunge wakichangia muswada huo walisema wakati wa kuvunjwa kwa TRL na Rahco, masilahi ya wafanyakazi yazingatiwe na kuhakikisha wanaobomolewa nyumba zao kupisha ujenzi, pia wanalipwa haki zao.

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe alisema kaya zipatazo 500 zinatakiwa kuhama kupisha ujenzi wa reli jimboni kwake na wapo ambao wameishi maeneo hayo kwa zaidi ya miaka 80.

Mbunge wa Igalula (CCM), Mussa Ntimizi alihoji kampuni ya reli ilikuwa wapi hadi wakawaacha watu kujenga ndani ya hifadhi ya reli.

Akizungumzia fidia, Profesa Mbarawa alisema mwananchi anayevamia barabara hawezi kulipwa fidia bali kama barabara imemfuata huyo atalipwa.