Kampuni za utalii zabanwa, zatakiwa kutoa mikataba ya ajira

Muktasari:

  • Kuanzia sasa kampuni ambayo wafanyakazi wake hawatakuwa na mikataba ya kazi, haitaruhusiwa kuendelea na shughuli zake

Arusha. Kampuni za kupandisha watalii mlima Kilimanjaro kuanzia sasa haziruhusiwi kuendelea na jukumu hilo kama hazitakuwa na mikataba ya kazi wafanyakazi wake wanaowaongoza watalii hao, wanaobeba mizigo yao na wapishi.

Mpaka kufikia mwaka 2018, kampuni takribani 200 zinazojihusisha na kupandisha watalii katika mlima huo zilikuwa zikiendesha shughuli hizo lakini nyingi wafanyakazi wake hawana mikataba ya ajira.

Uamuzi wa kutaka kampuni hizo kuwapa mikataba ya ajira wafanyakazi wake ulitolewa wiki iliyopita na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla na Idara ya Kazi.

Jana Juni 24, 2018 maofisa wa Idara ya kazi mkoa wa Kilimanjaro, wameanza ukaguzi wa mikataba hiyo ya kazi na kutoa mikataba kwa makampuni ambayo hayakuwa nayo kwenye malango ya kupanda Mlima Kilimanjaro.

Afisa Idara ya kazi mkoa wa Kilimanjaro, Arbert Ngendelo akizungumza na mwananchi jana alisema, wamechukuwa uamuzi huo, ili kutekeleza maagizo ya serikali na kutaka kutambuliwa rasmi kazi za wapagazi, wapishi na waongoza watalii.

"ni kweli vijana wanaofanyakazi hizi hapa mlimani wote walikuwa hawana mikataba hivyo, walikuwa wakikosa fedha zao na wengine kulipwa ujira mdogo tofauti na maagizo ya serikali lakini sasa watalipwa viwango ambavyo vinakubalika"alisema

Akizungumzia utekelezaji wa maagizo hayo ya Serikali, Katibu Mkuu wa chama cha wapagazi nchini(TPO), Loshiye Mollel alisema wanaipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kusikiliza kilio chao cha muda mrefu.

 

"kwa zaidi ya miaka 10 tumekuwa tukiomba tuwe na mikataba ya ajira japo ni ya muda lakini tulikwama sasa tunaishukuru sana serikali kuingilia kati na tayari tumeanza kuona makampuni makubwa ya utalii yamekubali kutoa mikataba"alisema

Hivi karibuni, muungano wa vyama vya waongoza watalii nchini, ulikutana na Viongozi wa wizara ya Maliasili na Utalii na viongozi wa wizara ya Kazi, Ajira na wenye ulemavu na kuomba serikali kuingilia kati ili walau wawe na mikataba ya ajira zao.

Kutokana na maombi hayo, Kaimu Kamishna wa Kazi, Lolegwa  Mkonya, aliagiza maafisa wa kazi mkoa wa Kilimanjaro, kuanza kazi ya kukagua mikataba ya ajira zoezi ambalo hadi sasa linaendelea.