Kamusi Kuu ya Kiswahili yazinduliwa

Muktasari:

  • Ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu) alipozungumza na wabunge, viongozi wa Serikali na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Kamusi Kuu ya Kiswahili uliofanyika kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa ustawi wa Taifa na katika kulinda umoja wa kitaifa.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu) alipozungumza na wabunge, viongozi wa Serikali na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Kamusi Kuu ya Kiswahili uliofanyika kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.

“Serikali inatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa ustawi wa nchi yetu na katika kulinda umoja wa kitaifa. Hakika lugha ya Kiswahili ndiyo inayotufanya tuwe Watanzania. Hivyo, tunaithamini na kwetu hii ni lulu na tunu ya Taifa,” amesema.

Waziri Mkuu katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake amesema uzinduzi wa kamusi hiyo unaenda sambamba na azma ya Serikali ya kutumia Kiswahili kwenye shughuli zote za kitaifa kama vile mikutano, mijadala, semina na ufundishaji shuleni.

Majaliwa amempongeza Rais John Magufuli kwa kuhimiza matumizi ya Kiswahili kwenye mikutano na matukio muhimu ya kitaifa, kama vile dhifa za kitaifa anazowaandalia wageni wake kutoka nje.

“Hata alipokuwa kwenye mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika, Rais alitumia Kiswahili kuhutubia mkutano huo. Amekuwa akifanya hivyo, hata kwenye mikutano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki lengo lake ni kuitangaza lugha hii ya Kiswahili,” amesema.

Amewasihi wazazi wahakikishe watoto wao wanapata kamusi hiyo kama moja ya nyenzo zao za kujifunza lugha ya Kiswahili.

“Ninashauri makundi mengine kama vile waheshimiwa wabunge, wanahabari, wakalimani, wafasiri, waandishi na wahariri wa vitabu, maofisa mawasiliano wa kwenye ofisi zetu, muone umuhimu wa kununua kamusi hii ili iwasaidie kujiimarisha kwenye matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu,” amesema.

Awali, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema Kiswahili ni lugha ya pili inayotumiwa na watu wengi zaidi barani Afrika lakini pia ni lugha ya 10 kati ya 6,000 zinazozungumzwa na watu wengi duniani.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), Dk Seleman Sewangi amesema kazi ya kuandaa kamusi hiyo ilianza Agosti 12, 2011 na kukamilika mwaka 2015 na toleo la kwanza lilichapishwa.

Amesema kamusi hiyo imekusanya maneno mengi makuu (vidahizo) kuliko kamusi zilizotangulia na kwamba ya sasa ina maneno 45,500.