Kanuni za maudhui ya kimtandao zamuibua Nape

Muktasari:

Asema jambo hilo linafikirisha

 


Dar es Salaam. Hatua ya baadhi ya wazalishaji na wasambazaji wa maudhui mitandaoni kulalamikia kanuni za maudhui ya kimtandao za mwaka 2018, kumemuibua mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye.

Wachapishaji wa maudhui katika blogu na majukwaa ya mtandaoni wanatakiwa kusajiliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kupata leseni kulingana na gharama zilizoanishwa.

Baadhi ya mitandao imedai kusitisha huduma hizo kutokana na tangazo la TCRA linalosema ni kosa kisheria kutoa huduma ya maudhui ya mtandaoni bila kuwa na leseni, hivyo kuanzia Juni 11, 2018 watoa maudhui hawaruhusiwi kuweka taarifa mtandaoni.

Nape aliyewahi kuwa Waziri  wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter huku akiambatanisha picha ya mkurugenzi mtendaji wa Mtandao wa Jamii Forum, Maxence Melo amesema, “Hili la JF (Jamii Forum) linafikirisha. Ukizuia watu kusema wayawazayo unaweza kutana nao..... kimya kimya!."

Mmoja wa watu waliochangia maoni ya mbunge huyo, akiwemo Goodluck Mayani amesema, “Nimeona kwenye 'status' za watu hii taarifa inayohusu Jamii Forum nikasema ngoja kidogo nikimbie Twitter kwa habari zaidi, ghafla nakutana na hii tweet yako@Nape Moses Nnauye

Naye Wilb-jr amesema, “yajayo yanafurahisha sana na tutaona mengi sana ila mheshimiwa ulikuwa sehemu ya kutungwa kwa sheria hizi ukiwa waziri leo hii inakuumaje kwa sheria husika kuanza kufanya kazi. Ipo siku na Twitter na Whatsapp nayo tutaikuta gizani maana maumivu huanza polepole."

Pia kanuni hizo zinaipa nguvu TCRA kudhibiti mawasiliano ya mtandaoni kwa kuchukua hatua kwa wasiotimiza wajibu ikiwamo kuamuru kuondolewa kwa ‘maudhui yasiyofaa’ na usajili wa watumiaji na majukwaa. Kanuni hzo zinatokana na Sheria ya Mawasiliano ya Kielekroniki na Posta ya mwaka 2018.