Kanye West agonganisha wasanii Uganda

Muktasari:

Rapa huyo wa Marekani yuko nchini Uganda ambako anatembelea miradi ya kijamii na pia kuchukua picha za video kwa ajili ya albamu yake mpya ya Yandhi.


Dar es Salaam. Wakati Bebe Cool ameituma ombi la kurekodi pamoja na nyota wa muziki wa rap duniani, Kanye West, msanii mwenzake, Bobi Wine amelaani kitendo cha Mmarekani huyo kukutana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

West yuko nchini Uganda na mkewe Kim Kardashian pamoja na binti yao, North West katika ziara yao inayohusisha kutembelea shughuli za kijamii na kurekodi video ya albamu yake mpya ya Yandhi.

Akitarajia ujio wa nyota huyo wa Marekani, Bebe Cool ambaye jina lake halisi ni Moses Ssali, aliandika katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii akimuomba West afanye collabo na msanii mzawa wa Uganda.

Bebe Cool (41) alijua kuwa ujumbe wake utamfikia Mmarekani huyo ambaye ana umri wa miaka 41.

Na wakati akitembelea kituo cha Jitihada za Wanawake wa Uganda Kuokoa Watoto Yatima (Uweso) jana, Kanye West alizungumzia mpango wake wa kufanya kazi na wasanii wazawa ili kusaidia kukuza muziki wa Uganda.

Gazeti la The Daily Monitor limemkariri Kanye akizungumzia mpango huo baada ya kuulizwa swali kama yuko tayari kushirikiana na wasanii wa Uganda katika moja ya ziara zake.

“Uganda ni nchi nzuri sana na tutarudi. Tutafanya kazi na wanamuziki wa Uganda kukuza muziki wao,” alisema Kanye ambaye alikuwa ameambatana na Kim nyota wa vipindi vya mazungumzo vya televisheni, Godfrey Kiwanda (Waziri wa Mambo ya Ndani), Hillary Onek (Waziri wa Kukabiliana na Majanga, Misaada na Wakimbizi) na viongozi wengine wa Serikali.

Pia alisema atasaidia watoto yatima wa kituo hicho na baadaye kugawa raba za chapa ya Yeezy pamoja na fulana.

“Tutarejea kufanya kazi na kijiji cha watoto cha Uweso kuhakikisha kuwa watoto wanapata maisha mazuri,” alisema.

Kabla ya kutembelea kijiji hicho, Kanye West alikwenda Ikulu ambako alifanya mazungumzo na Rais Museveni ambaye baadaye aliwapa helikopta ya jeshi kwenda Uweso.

Lakini mazungumzo yake na Rais Museveni hayakumpendeza Bobi Wine, mwanamuziki aliyegeukia siasa na kuwa kinara wa upinzani dhidi ya Serikali ya mwanasiasa huyo mkongwe.

Wine ambaye ni nyota wa muziki wa reggae alimshambulia West baada ya Rais Museveni kutoa picha zinazomuonyesha akiwa na mwanamuziki huyo nyota wa Marekani na baadaye akikabidhiwa raba zenye chapa ya Yeezy.

Museveni ambaye sasa ana umri wa miaka 74 alijibu mapigo kwa kukabidhi West kitabu alichosaini cha Sowing the Mustard Seed: The Struggle for Freedom and Democracy in Uganda (Kupanda Mbegu: Harakati za Uhuru na Demokrasia Uganda).

Museveni alisema amefurahia mazungumzo hayo na West akisema yalikuwa na mafanikio.

Lakini Bobi Wine, Mbunge na mwanamuziki maarufu wa Afrika Mashariki alisema haikuwa sahihi kwa West kutumia sauti yake ‘kupapasa mabega ya Rais’.

Wine ambaye alikamatwa na kuumizwa akiwa mahabusu alisema: “Anaongea na Rais ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 32 na amezuia uhuru wowote, nchi ambayo wapinzani wanateswa na kufungwa.”

Watu watatu waliuawa na karibu wengine 100 walikamatwa katika vurugu zilizotokea baada ya Wine kukamatwa. Zaidi ya watu 80 ambao ni wasanii, wanaharakati na wanasiasa wamesaini tamko la kulaani vitendo alivyofanyiwa Wine. Waliosaini ni pamoja na Chris Martin, Chrissie Hynde, Brian Eno na Damon Albarn, pamoja na wanamuziki wengine maarufu barani Afrika kama Femi Kuti.

“Ingekuwa kitu bora kama angetumia sauti yake kwa ajili ya mambo mazuri ya watu wa Afrika,” alisema Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi.

“Mimi ni mwanamuziki lakini siruhusiwi kufanya onyesho lolote katika nchi yangu kwa sababu nampinga Rais. Inaudhi.”

West ametuma video kwenye mitandao ya kijamii kuelezea safari yake barani Afrika na kumuelezea Fela Kuti, gwiji mtata wa muziki wa Nigeria ambaye ni mtunzi na mwanaharakati aliyefariki mwaka 1997 kama mtu ambaye amekuwa akimuhusudu.