Kardinali Pengo aonya injili zinazolenga kuwapa watu utajiri, miujiza

Muktasari:

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo awaonya waumini wa kanisa hilo kuhubiri injili zenye mlengo wa kutoa miujiza na utajiri

Dar es Salaam. Askofu Mkuu  wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewataka waumini wa kanisa hilo kuacha kudanganywa na watu wanaoibuka na kutangaza injili  inayolenga kuwapatia utajiri na kutenda miujiza.

Pengo amesema hayo leo Jumapili wakati wa Misa ya Kipaimara kwa watoto 65   iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Padri Pio Tabata Kisiwani jijini humo.

Ibada hiyo pia imeenda sambamba na maadhimisho ya sherehe ya msimamizi mkuu wa  Parokio hiyo, mtakatifu Padri Pio.

Katika mahubiri yake, Kardinali Pengo amesema nyakati za hivi karibuni kumekuwa na makundi ya watu ambao wanadai kutoa miujiza ya kufufua wafu na wengine kutoa utajiri na kudai kuwa mwenye uwezo huo alikuwa Yesu pekee na siyo watu.

"Leo  kuna watu wanatangaza injili   za kuleta utajiri na kutenda miujiza, nawaomba waumini na ninyi wote ambao leo mnapokea kipaimara, katangazeni injili thabiti ambayo italeta amani, upendo na kuutukuza utukufu wa Mungu ndani yenu," amesema.

Pengo amesisitiza waumini kumtukuza Mungu na kutenda yale yanayompendeza muda wote hata kama watakuwa maskini au watakuwa na matatizo na kuonya utajiri wa mali za dunia usiwe ndiyo chanzo cha  kumtukuza Mungu au kikwazo cha kutomtukuza.

Amesema kuhubiri injili yenye mlengo wa kupata utajiri na kutenda miujiza wakati ndani ya mioyo ya watu kumejaa dhambi bado si kitu mbele za Mungu na siyo kusudi la Mungu.

"Mimi, wewe na ninyi hatuna uwezo wa kufanya miujiza kama Yesu, tukumbuke Mungu aliponya watu kama ishara ya ukuu wake ndiyo maana aliponya wachache" amesema.

"Ikitokea tumekufa Mungu hatatuuliza tulikuwa na mamilioni mangapi bali atatuuliza ni vipi tumeudhihilisha ukuu wake kupitia matendo na mioyo yetu katika kutangaza neno lake."