Kashfa yaibuka kwa watumishi wa TRA bandarini

Muktasari:

  • Watumishi hao wamekuwa wakiwatoza kiwango kikubwa cha ushuru wa bidhaa tofauti na kinachoandikwa kwenye stakabadhi, huku wakiwatishia kuchukua mizigo wanaposhindwa kutekeleza.

Dar es Salaam. Watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kitengo cha Bandari ya Dar es Salaam wanalalamikiwa kuwabambikia wananchi ushuru usioendana na uhalisia wanapotoa bidhaa Zanzibar na kuingia nazo Bara.

Watumishi hao wamekuwa wakiwatoza kiwango kikubwa cha ushuru wa bidhaa tofauti na kinachoandikwa kwenye stakabadhi, huku wakiwatishia kuchukua mizigo wanaposhindwa kutekeleza.

Mmoja wa waathirika wa kadhia hiyo ni Estabella George aliyekuwa akisafiri kutoka Zanzibar kuja Dar es Salaam akiwa na televisheni yenye ukubwa wa nchi 50 aliyoinunua kwa Sh600,000.

“Nilipofika bandarini waliniuliza risiti, nikawapa. Wakaniambia nilipe ushuru Sh400,000 nikakataa; niliwauliza nawezaje kununua televisheni kwa Sh600,000 halafu nilipe tena Sh400,000.

“Tulibishana na kuvutana, ikanibidi nimpigie mama yangu ambaye naye alishangazwa. Kwa kuwa sikutaka usumbufu, na wao walipoona ninakomaa wakasema niwape laki tatu, nikakataa, nikawaambia nikiwapa mtanipa na risiti ya EFD (ya kielektroniki), wakasema ndiyo.”

Estabella alisema baada ya kuwaeleza wampatie risiti ya EFD, watumishi hao waliingia ndani kujadiliana na waliporudi walimtaka awapatie Sh200,000.

“Sikuwa na fedha, nikawaambia niiache televisheni kwa kuwa nilikuwa nawahi, wakakubali nikaiacha; hiyo ilikuwa Ijumaa nilipokwenda kesho yake Jumamosi (Machi 3), wakaniambia niwape Sh150,000. Kama ilivyokuwa awali nikawaambia wanipe risiti, wakakubali,” alisema Estabella.

“Nilipokwenda kuchukua risiti, nilikuta imeandikwa Sh75,476, nilipouliza nikajibiwa unataka mali yako au hutaki? Kwa kuwa nilikuwa naona nachelewa na usumbufu unazidi nikachukua mzigo wangu nikaondoka lakini pale bandarini kuna tatizo kubwa, sikuwa mimi peke yangu na wengine walikuwapo wanalalamika na nilijaribu kuchungulia eneo wanalohifadhi mizigo, inaonekana abiria wengi wanaisusa baada ya kutajiwa kodi kubwa,” alisema.

Salim Said aliyekuwa bandarini Jumamosi iliyopita aliyesafiri kwa boti ya saa nane mchana pia alilalamikia kadhia hiyo.

Said alisema alibeba pasi ya umeme na alitakiwa kutoa ushuru wa Sh70,000 ambao aligoma kulipa na kuamua kuiacha na kuondoka.

Alipofuatilia, mwandishi wetu alibaini kuwapo malalamiko kutoka kwa wasafiri wengi katika ulipaji ushuru wa bidhaa wanazonunua Zanzibar na kuingia nazo Bara.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo aliomba kutumiwa risiti za Estabella kwa hatua zaidi ambazo alitumiwa.