Kata umeme aliyoagiza JPM yaondoa huduma Muguwasa

Muktasari:

  • Kaimu meneja wa Tanesco Wilaya ya Serengeti, Peter Mtete alisema wamefikia uamuzi wa kuikatia umeme Muguwasa kutokana na malimbikizo ya deni la Sh19 milioni. Hatua hiyo imesababisha wakazi zaidi ya 50,000 wa mji wa Mugumu na vitongoji vyake kukosa huduma ya majisafi na salama tangu Oktoba 19.

Agizo la Rais John Magufuli kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) la kuwakatia umeme wadaiwa sugu zikiwamo taasisi za umma, limeanza kung’ata wilayani hapa baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mugumu (Muguwasa) kukatiwa kutokana na deni la Sh19 milioni.

Kaimu meneja wa Tanesco Wilaya ya Serengeti, Peter Mtete alisema wamefikia uamuzi wa kuikatia umeme Muguwasa kutokana na malimbikizo ya deni la Sh19 milioni. Hatua hiyo imesababisha wakazi zaidi ya 50,000 wa mji wa Mugumu na vitongoji vyake kukosa huduma ya majisafi na salama tangu Oktoba 19.

Akizungumzia kadhia hiyo, kaimu meneja wa Muguwasa, Shukrani Tungaraza alisema wamelipa Sh5 milioni kati ya fedha wanazodaiwa na wameomba kurejeshewa huduma wakati juhudi za kukamilisha malipo ya Sh14 milioni zikiendelea.

Wakati Muguwasa ikielezwa kukusanya kati ya Sh9 hadi 10 milioni kwa mwezi kutoka kwa wateja wake zaidi ya 1,600, gharama ya umeme pekee inaigharimu Sh12 milioni kwa mwezi. Mkazi wa Mugumu, Ghati Wambura aliishauri halmashauri ya wilaya kuangalia namna ya kusaidia uendeshaji wa Muguwasa.