Katibu Bunge ahoji haki za Lissu

Muktasari:

Kauli hiyo inayoweza kuibua malumbano mapya katika matibabu ya mwanasheria huyo mkuu wa Chadema, imetolewa siku mbili baada ya Lissu kuhoji sababu za Bunge kutojihusisha na matibabu yake tofauti na sheria zinavyotaka.

Dar/Dodoma. Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai amesema amemwandikia barua kaka wa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, akimtaka alieleze ni stahiki zipi ambazo ndugu yao anastahili apewe na chombo hicho.

Kauli hiyo inayoweza kuibua malumbano mapya katika matibabu ya mwanasheria huyo mkuu wa Chadema, imetolewa siku mbili baada ya Lissu kuhoji sababu za Bunge kutojihusisha na matibabu yake tofauti na sheria zinavyotaka.

Lissu yuko Hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako anatibiwa tangu Septemba 7 aliposhambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana wakati waki ndani ya gari lililoegeshwa nje ya makazi yake mjini Dodoma.

Kauli ya Lissu ilikuwa ni mwendelezo wa kilio kilichotolewa awali na ndugu yake, Alute Mughwai Lissu ambaye alisema alishaiandikia ofisi ya Bunge kutaka ilipie gharama za matibabu ya mbunge huyo.

Katika mahojiano na Mwananchi hospitalini jijini Nairobi, Lissu alisema alimwambia Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ahoji “Bunge liko wapi” kutokana na kutofanya juhudi za kwenda kumuona tangu alazwe takriban miezi mitatu iliyopita.

Pia alieleza kushangazwa na kitendo cha chombo hicho kutogharimia matibabu ambayo anastahilki kisheria iwe anatibiwa ndani au nje ya nchi.

Lakini jana, alipoulizwa kuhusu hatua waliyofikia baada ya kupokea barua ya familia hiyo iliyotaka Bunge lizingatie haki za msingi za ndugu yao, Kagaigai alionekana kutaka maelezo kutoka kwa familia.

“Sisi tumewajibu hizo haki ni zipi kwa sababu kuna allowance (posho) kuna mshahara zote hizo ni haki za mbunge. Hajajibu haki anazoongelea ni zipi,” alisema Kagaigai ambaye alimtaka mwandishi wa Mwananchi asimrekodi sauti yake na baadaye kuandika maelezo hayo katika daftari lake.

Kigaigai alisema barua hiyo imeandikwa na Bunge Jumatatu (Novemba 27) na kwamba bado wanasubiri majibu kutoka kwa Alute kuhusu haki anazotaka Bunge izingatie.

Alipotafutwa azungumzie majibu hayo ya katibu wa Bunge, Alute ambaye kitaaluma ni wakili wa kujitegemea, alisema hajapata barua hiyo ya ofisi ya Bunge.

“Mpaka sasa (saa 7:00 mchana) sijapokea barua yoyote.”

Kuhusu haki hizo, Alute alisema kama ambavyo alizungumza huko nyuma kwamba sheria inamtambua Lissu na hivyo anatakiwa agharimiwe matibabu yake.

“Lissu si wa kwanza au wa mwisho kutibiwa nje. Matibabu ya mbunge kwani ndio yanaanzia Lissu?” alihoji.

“Yanatambulika kisheria kwa hiyo sijajua hiyo barua imetutaka kufanya nini. Ngoja tuisubiri.

“Hivi (aliyekuwa mbunge wa Songea Mjini-CCM, marehemu) Leonidas Gama alivyokwenda India, alijipia au aligharamiwa na Bunge?”

Katika mahojiano kati na Mwananchi jijini Nairobi, Lissu alisema kwa wadhifa wake wa ubunge na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni anatambuliwa na sheria za Tanzania hususan Sheria ya Uedeshaji wa Bunge na kugharamiwa matibabu si hisani bali ni stahiki zake.

Alisema sheria hiyo inaeleza mbunge anapoumwa atapata matibabu pamoja na gharama nyingine kutoka bungeni pamoja na mtu anayemuuguza ambaye hulipwa nusu ya posho ya mbunge ili kumudu gharama za maisha.

Alisema hilo hufanyika baada ya mgonjwa kuwa amelazwa nje ya eneo la Bunge, akimaanisha Dodoma na bila ya kujali anatibiwa Dar es Salaam, Afrika Kusini, India Marekani au Kenya.

Lissu alisema Spika wa Bunge, Job Ndugai anajua kwamba aliumizwa na ndiyo maana aliwahi kulitangazia Bunge na akaendesha shughuli ya kumchangia ingawa alishangazwa na ukimya wa yeye kutopewa stahiki zake na kuahidi akitoka atazipigania kwani ni haki zake.

Septemba 21, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga kuhusu gharama za matibabu ya Lissu, alisema Serikali haijashindwa wala haijakataa kumhudumia.

“Lissu ni Mtanzania na ni mbunge,” alisema.

“Hata sasa hivi anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Nairobi, lakini kidogo tunaona kunafanyika mambo tusiyoyaelewa kama dhamira ya kufanyika kwa mambo hayo.

“Muwaeleze Watanzania na familia kwamba Serikali iko tayari kumhudumia Lissu popote anapotaka kupelekwa duniani iwapo tutapata maombi rasmi kutoka kwa familia.”

Ufafanuzi wa Waziri Mwalimu ulitofautiana na ule alioutoa Spika wa Bunge, Job Ndugai Septemba 15 bungeni mjini Dodoma wakati akijibu tuhuma za wabunge, hususan wa upinzani waliodai Bunge limeshindwa kumgharamikia Lissu.

Ndugai alisema baada ya kueleza kwamba utaratibu wa bima wanayotumia ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ni wa kutibiwa katika hospitali za Serikali.

“Sisi wote tuna bima pamoja na mawaziri na bima yetu inafanana na ni NHIF. Bima yetu tunatibiwa katika hospitali hii yetu ya mkoa au hospitali nyingine za Serikali, rufaa yetu ni Muhimbili. Baada ya hapo ni kupelekwa India Hospitali za Apollo,” alisema Spika.