Katibu wa Chadema Nachingwea ajiunga na CCM

Muktasari:

Waziri Mkuu alipokea kadi nne za CUF, moja ya ACT na mbili za Chadema kutoka kwa wanachama hao saba kabla hajawakabidhi kadi za CCM.

Ruangwa. Katibu Mwenezi wa Chadema Kata ya Nachingwea, Ismail Hamisi amejiunga na CCM na kumkabidhi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kadi yake.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amepokea wanachama saba kutoka vyama vitatu vya upinzani ambao wameamua kurejea CCM na wengine 82 kutoka CUF.

Wanachama hao wamepokewa leo Ijumaa, Mei 25, 2018 wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua uwanja mpya wa michezo unaojengwa katika Kijiji cha Dodoma, Kata ya Nachingwea, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.

Waziri Mkuu ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alipokea kadi nne za CUF, moja ya ACT na mbili za Chadema kutoka kwa wanachama hao saba kabla hajawakabidhi kadi za CCM.

Wanachama hao saba waliokabidhiwa kadi mpya za CCM pamoja na wenzao 82, walikula kiapo cha uaminifu mbele ya Waziri Mkuu.