Kauli ya Nape yaibua upya hoja ya mgombea binafsi

Muktasari:

Mwaka 1993, Mchungaji Christopher Mtikila alifungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma iliyosikilizwa na Jaji Kahwa Lugakingira akitaka kutambuliwa kwa mgombea binafsi.

Dar es Salaam. Kauli ya mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye kwamba mtu akihama chama ahame na uwakilishi wake imeibua tena hoja ya kuwapo mgombea binafsi.

Mwaka 1993, Mchungaji Christopher Mtikila alifungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma iliyosikilizwa na Jaji Kahwa Lugakingira akitaka kutambuliwa kwa mgombea binafsi.

Jaji Lugakingira ambaye kama ilivyo kwa Mchungaji Mtikila wote ni marehemu, alikubaliana na hoja kwamba kugombea kama mtu binafsi ni haki ya kila raia kwa mujibu wa Katiba, kwa maana ya haki ya kuchagua viongozi na haki ya kugombea uongozi.

Hata hivyo, mwaka 1994 hoja hiyo ilikwama bungeni baada ya chombo hicho kufanya mabadiliko ya 11 ya Katiba katika Ibara ya 34 kwa kuzuia wagombea binafsi.

Mwaka 2005, Mchungaji Mtikila alifungua tena kesi Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam akipinga marekebisho hayo ya Katiba na jopo la majaji watatu, chini ya Amiri Manento (akiwa Jaji Kiongozi) lilikubaliana na hoja za mlalamikaji na kuruhusu mgombea binafsi. Lakini mwaka 2010, Serikali ilikata rufaa Mahakama ya Rufaa ambako majaji saba chini Jaji Mkuu wakati huo, Augustino Ramadhani walisema hakuna mahakama yoyote nchini yenye uwezo wa kisheria kusikiliza kesi inayotaka mgombea binafsi na kwamba mahakama za chini zilijipachika madaraka ya kibunge ya kutunga sheria badala ya kuzitafsiri.

Jana, wanasiasa na wasomi waliozungumza na Mwananchi kuhusu kauli ya Nape waliibua hoja ya mgombea binafsi wakisema wagombea watakuwa huru pasipo kikwazo.

Agosti 16, Nape akizungumza wakati wa mafunzo ya siku mbili ya kamati ya uongozi, makamu wenyeviti wa kamati za Bunge na wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge, alisema ifike mahali iruhusiwe mtu akihama chama ahame na ubunge au cheo alichonacho.

Akizungumzia kauli ya Nape, Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Ngemela Lubinga alisema haiwezekani kwa sababu uwakilishi ni mali ya chama na si mtu.

Huku akimtaka Nape kuweka wazi kama ana ajenda nyingine ya siri ili ifahamike, Lubinga alisema haiwezekani hata kubadilisha sheria kwa sababu suala hilo lina mkanganyiko.

Alisema itikadi ya chama ndiyo inakifanya kishinde uchaguzi, hivyo kuhama na uwakilishi ni kuwanyima haki wapigakura waliomchagua kwa itikadi ya chama chake.

Alisema ubunge au udiwani ni mali ya chama, hivyo mtu hawezi kuhama na wadhifa wake kwa sababu si mali ya chama anachohamia.

“Jambo hili linaeleweka, halihitaji staretegic analysis (uchambuzi wa kimkakati). Atuambie kama ana ajenda ya siri,” alisema Lubinga.

Akiwa na mtazamo kama huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (Out), Hamad Salim alisema kuhalalisha wabunge au madiwani kuhama na vyama na vyeo vyao kutaondoa nguvu ya wananchi kuchagua viongozi na kwamba wanasiasa wataendelea kufanya mchezo huo kila wanapojisikia.

“Nadhani utaratibu uliopo unafaa na unakidhi matakwa. Tuangalie vyanzo vingine vya hawa wanaohama ni nini. Pia, tunaweza kujadili mahitaji ya kuwa na wagombea binafsi,” alisema Salim.

Hata hivyo, aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Felix Kibodya alisema kuna umuhimu wa kuruhusu wagombea binafsi ili watakaohamia chama kingine wahame na nafasi zao, “Kikatiba na kisheria hili haliwezekani, lakini tungekuwa na watu independent (huru), ingewezekana. Lazima element ya kuchaguliwa iwepo ndipo mtu awe mbunge au diwani na si kuhama tu.”

Akiwa na mtazamo kama huo, mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Benson Bana alisema sasa ni wakati wa kuruhusu wagombea binafsi kwa sababu kuna watu ambao wako kwenye vyama kwa sababu ya kutimiza matakwa ya kisheria lakini mioyo yao haipo huko.

Alisema hoja ya muhimu kwa sasa si kuhama na ubunge, bali kujiuliza ni kwa nini watu hao wanahama kutoka chama kimoja kwenda kingine na kupewa nafasi tena ya kugombea huko.

“Lazima turuhusu mgombea huru, kuna watu wana ushawishi na wangependa kujidhamini wenyewe lakini kwa sababu ya matakwa ya kisheria wanalazimika kujiunga na vyama vya siasa.”

Dk Bana alisema baadhi ya wabunge hao ndio wanaovihama vyama vyao wakihofia hatima yao ya kisiasa kuelekea uchaguzi wa mwaka 2020.

Alisema wanasiasa wanapima upepo na kuamua kuvihama vyama vyao ili kutengeneza mazingira mazuri ya uchaguzi ujao.