Kauli ya Obama yakamata

Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama akihutubia katika mhadhara wa kumbukumbu ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela wiki hii. Picha na mtandao


Muktasari:

Lubinga alikuwa mmoja wa wanasiasa na wanadau waliohojiwa na Mwananchi kuhusu kauli ya kiongozi huyo wa taifa kubwa duniani aliyoitoa wakati wa sherehe za kumbukumbu ya rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.

Dar es Salaam. Ngemela Lubinga, katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM anayehusika na uhusiano wa kimataifa, amekubaliana na kauli ya rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama kuwa viongozi wengi Afrika hawafuati katiba na wanaongoza kwa mabavu.

Lubinga alikuwa mmoja wa wanasiasa na wanadau waliohojiwa na Mwananchi kuhusu kauli ya kiongozi huyo wa taifa kubwa duniani aliyoitoa wakati wa sherehe za kumbukumbu ya rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.

Lubinga alikuwa mmoja wa watu waliokubaliana na Obama kuhusu mwenendo huo wa viongozi wa Afrika, bara ambalo limepitia katika utumwa, ukoloni, mapinduzi ya watawala na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Obama alisema baadhi ya viongozi wa Afrika wanakandamiza demokrasia na kwamba siasa za kutia watu hofu, misimamo mikali na hali ya kutoridhika zinashika kasi barani Afrika.

Alisema inaonekana ni kama dunia inaelekea kwenye siasa za kukaripiana na kwamba ni lazima kuwa macho dhidi ya watu wanaojaribu kujitukuza kwa kuwashusha hadhi wengine.

Akizungumzia kauli ya Obama, Lubinga alisema kuna baadhi ya viongozi hawafuati demokrasia, wanadharau katiba, hawaitishi uchaguzi na wanaongoza kwa mabavu.

Lubinga alisema anakubaliana na Obama kwa sababu ni kweli kuna sehemu za Afrika demokrasia haiheshimiki.

“Ni kweli baadhi ya wenzetu hawafuati demokrasia, katiba zinadharaurika na hakuna uchaguzi, viongozi wanaongoza kwa mabavu huku wengine wakijiongezea muda wa kutawala bila kufuata utaratibu,” alisema mstaafu huyo wa jeshi.

Lubinga: Wananchi wapiganie haki

Lakini Lubinga hakuishia hapo, bali alishauri njia ya kuondoka na viongozi wa aina hiyo.

“Wananchi wenyewe waongee na kupigania haki yao, lakini wasitumiwe na watu, kikundi au taasisi yoyote,” alishauri Lubinga.

“Jambo jingine ni kwa viongozi wenyewe kuheshimu katiba na kusimamia mambo ya msingi kama suala la uchanguzi ili kutoa haki ya kuchagua au kuchaguliwa kwa lengo la kuwa na wawakilishi bungeni.”

Maoni kama hayo yalitolewa na Dk Benson Bana, mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DSM). “Ingawa Obama anaonekana kuakisi maisha ya nchi yake, ukweli ni kwamba alichoongea kipo pia Afrika. Ni haki yake kukosoa,” alisema Dk Bana.

Bana alisema ujumbe huo umefika na kwamba utakuwa fundisho hata kwa wale wanaotawala kwa ubabe baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi ambao haukuwa na mazingira sawa ya ushindani.

“Ujumbe ni mzuri,” alisema.

“Ingawa hajataja nchi, lakini kuna baadhi ya nchi zetu za Afrika zina udikteta na utawala wa kiimla kwa kiasi kikubwa, jambo linalochangia kuminya demokrasia,” alisema.

Bana alitaka kila kiongozi atafakari ujumbe huo.

Kuondolewa ukomo wa umri

Mwingine aliyekuwa na msimamo kama huo ni mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Shoo Innocent aliyesema viongozi wa Afrika ni kikwazo cha demokrasia.

“Ingawa safari hii hakutaka kutaja hasa ni viongozi gani, lakini alichokisema hata sisi Waafrika kinatuhusu,” alisema.

“Tunashuhudia Uganda na Burundi jinsi walivyotoa suala la umri katika nafasi ya urais. Lakini tumeshuhudia kilichotokea Zimbabwe hadi kufikia hatua ya kufanya mapinduzi baridi. Sudan Kusini ni mfano mbaya wa vita vinayosababishwa tu na viongozi kutoheshimu demokrasia.”

Innocent alisema njia pekee ya kujikwamua ni kuupa nguvu Umoja wa Afrika, akisema kwa sasa hauna meno jambo linalochangia nchi wanachama kushindwa kuuheshimu.

“Hiki ndiyo chombo cha juu kwa Waafrika kukutana na kutatua matatizo yetu, lakini ilivyo sasa imebaki kuwa tu sehemu ya kufanya mikutano na washiriki kufanya shopping (ununuzi) pekee. Hakiko strong (imara),” alisema.

“Ni lazima bajeti ya chombo hiki iimarishwe kwa wanachama wake kuchangia asilimia kadhaa.”

Mhadhiri huyo wa masuala ya diplomasia alisema njia nyingine ni kwa nchi za Afrika kuwa na jeshi imara ambalo litatoa msaada pindi unapohitajika badala ya kusubiri kuomba msaada kwa nchi za Magharibi.

“Jambo jingine ni viongozi wenyewe waheshimu demokrasia, kusimamia utawala bora pamoja na kusimamia ipasavyo katiba za nchi zao.”

Pia alishauri kupunguza vikwazo na vipingamizi katika masuala mbalimbali kama biashara na muingiliano katika suala la forodha.

“Lakini hayo yote hayawezi kufanikiwa bila kuwa na elimu bora ambayo itaenda sambamba na maisha ya sasa,” alisema.

“Pia siasa zetu zisiwe za mgawanyo na kikabila, tuache mila za kizamani ambazo zimepitwa na wakati ikiwa ni pamoja na kuwapa nafasi sawa wanawake katika masuala mbalimbali ya nchi.”

Katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alishukuru kwamba viongozi wakubwa duniani wenye jukumu la kusimamia na kulinda amani, wanaona jinsi ambavyo viongozi wenzao hawatendi haki huku wakitamba kuwa wanatetea wanyonge.

Dk Mashinji alisema kauli ya Obama iwe ndiyo njia ya viongozi wengine hasa Tanzania kuzingatia na kusimamia demokrasia na kuacha ubabe.

“Wayachukulie kwa uzito maneno yake na kuyafanyia kazi, haiwezekani leo kiongozi Afrika anajitangaza kuwa ameshinda kwa asilimia 90 kana kwamba hakukuwa na ushindani,” alisema daktari huyo wa binadamu.

“Hii inawezekana tu kwa viongozi ambao hawatoi ushindani sawa na haya tumeyashuhudia hata hapa kwetu.”

Naye John Mrema, mkurugenzi wa itifaki na mawasiliano ya mambo ya nje wa Chadema, alisema alihusisha kauli ya Obama na kinachoendelea nchini.

“Hata Tanzania mambo haya yanafanyika,” alisema.

“Sasa tumerudi nyuma tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, chaguzi zinafanyika bila kuzingatia haki za wengine. Lakini kukubwa zaidi viongozi hawana hofu.”

Mrema aliwataka viongozi wa Afrika wafikirie kama watapenda kutendewa haya wanayoyatenda sasa siku watakapokuwa wastaafu.

Mrema alisema hatari anayoiona ni kwa watu kuchoka utawala wa aina hiyo na kuchukua hatua zinazoweza kuigharimu.

“Ukiwatendea ubabe na kuwafunga midomo, watu wanatafuta njia mbadala ya kupumua. Chonde chonde wasiwalazimishe watu kufika huko kwani si pazuri,” alisema.