Kauli ya Sirro kuhusu utekwaji wa Mo Dewji yazua mjadala mtandaoni

Muktasari:

Maswali yaibuka baada ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kutoa taarifa za uchunguzi juu ya kutekwa kwa Mo Dewji ikiwamo kubaini gari walilotumia watekaji


Dar es Salaam. Baada ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kueleza hatua za uchunguzi juu ya kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ ikiwamo kubaini gari iliyotumiwa na watekaji kumeibua mjadala mzito mtandaoni.

Wanasiasa,  wanaharakati na wananchi wamehoji maswali mbalimbali kuhusu ufafanuzi huo wa Sirro.

Leo Oktoba 19 katika mkutano wake na waandishi wa habari, Sirro alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea huku akibainisha kuwa gari iliyotumika kumteka ‘Mo Dewji’ ina namba za nje ya Tanzania na kuzitaja kuwa ni AGX 404 MC.

“Tumefanya kazi kubwa kuhakikisha pale ilipopotelea tunapapata. Uchunguzi unaonyesha gari limetokea nchi jirani na watu wetu wamekwenda mpaka mpakani na kuona gari ya mwonekano huo ilipita Septemba Mosi,” alisema.

Mbali na gari, IGP Sirro alisema wamebaini aina ya risasi zilizotumika wakati wa tukio hilo lilitokea Oktoba 11 katika hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam ambako Mo Dewji alikwenda kufanya mazoezi.

Mjadala waibuka

Kufuatia ufafanuzi huo wa Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ni miongoni mwa waliohoji.

“...taratibu za gari kupita mpakani zinatia mashaka makubwa kauli ya IGP. Polisi na vyombo vya usalama nchini hutumia plate number (namba za gari) za kigeni. Ile picha ya gari sio ya CCTV. Kamanda Sirro Hapana,” amesema Zitto.

Kwa upande wake, Lema amesema: “Moyo wangu unavuja damu. IGP hapa ni collesium hoteli kweli.”

Mwanamitindo maarufu nchini, Flaviana Matata ameandika: “Watekaji hamjamaliza tu kufanya mlichotaka mturudishie mtu wetu jamani? Tuna amini mnaona vilio vyetu, please #BringBackMo #BringBackOurMo.”

Mwanahabari na mwanaharakati, Maria Sarungi Tsehai ameandika: “Bado naendelea na ku-process information ya press conference (mkutano wa waandishi wa habari)  ya leo kila nikiingiza data napata ERROR message. Naomba nirudi nikipata source of ERROR na nijue ERROR namba ngapi #BringBackMO #ChangeTanzania.”

Naye Martin M.M ameandika: “Mambosasa anasema tofauti kuhusu CCTV (zimeonesha wazungu, gari halikuonekana kabisa), Sirro anasema tofauti kuhusu hizo makamera za CCTV (gari imeonekana na dereva amejulikana na mmiliki wa gari, imetoka nchi jirani). “

Katika mkutano wake,  IGP Sirro aliwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa zinazoweza kusaidia kupatikana kwa ‘Mo Dewji’.

“Ni vizuri kujilinda na niwaombe tupeane taarifa za kweli na si za majungu na kuumiza mwingine. Mtu anasema Mo yupo hapa, unakwenda, unatumia mbwa, askari, magari hukuti mtu,” aLIsema.

Hadi sasa watu nane kati ya 27 waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo lililovuta hisia za watu wengi ndani na nje ya nchi bado wanashikiliwa kwa uchunguzi.