Kaya maskini kuchangia kuinua uchumi wa viwanda

Muktasari:

Swali: Serikali ya Rais John Magufuli imejielekeza katika kufanikisha Tanzania ya viwanda. Je, Tasaf imejipanga vipi kuhakikisha wanachangia kukuza uchumi wa viwanda.

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) ulioanzishwa 2000 kwa lengo la kupambana na umaskini uliokithiri uko katika awamu ya tatu (Tasaf III) ya utekelezaji wake. Mwandishi wetu, Noor Shija alifanya mahojiano na Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Ladislaus Mwamanga.

Swali: Serikali ya Rais John Magufuli imejielekeza katika kufanikisha Tanzania ya viwanda. Je, Tasaf imejipanga vipi kuhakikisha wanachangia kukuza uchumi wa viwanda.

Jibu: Tasaf inahusika na watu wa chini, watu maskini wenye kipato kidogo, lakini tunawajengea uwezo ili washiriki kwenye shughuli za kiuchumi ambazo zinagusa sekta mbalimbali. Kuna wanaojishughulisha na ufugaji, kilimo na biashara ndogo ndogo kwa kuwa siasa

za sasa za nchi yetu ni uchumi wa viwanda, hawa ni chanzo muhimu cha kutoa malighafi za viwandani. Hivyo, ni muhimu kuwajengea uwezo zaidi utakaowawezesha kutambuliwa bidhaa zao na kupata soko.

Hivyo, changamoto kwa viwanda vilivyopo na vingine vitakavyoongezeka vitahitaji malighafi kwa kuwa walengwa wa Tasaf wengi wanafanya shughuli za uzalishaji kama vile usindikaji watakuwa chanzo kizuri kwa kutoa malighafi za viwandani.

Mfano, kuna wanaoshughulika na biashara ya asali na wengine alizeti katika uzalishaji wa mafuta ya kupikia. Hivyo, wanufaika hao watahitaji kusaidiwa kuboresha viwango vya bidhaa zao ili waweze kupata fursa ya masoko na mtandao mkubwa wa kibiashara. Mpango huu wa Tasaf kwa kiasi kikubwa unashirikisha sekta zote kuanzia ngazi ya chini mpaka ya kitaifa, lengo lake ni kuifanya nchi iwe na maendeleo yanayomuhusisha kila mmoja na makundi yote.

Kwa hiyo, niseme tuko pamoja na wazo la Rais John Magufuli la Tanzania ya viwanda kwa kuunga mkono hilo sisi huku tunajihusisha katika kuwezesha ngazi za kiuchumi za chini ambazo zinagusa sekta zote kwenye ufugaji, kilimo na usindikaji kinachotakiwa ni kuongeza ubora, thamani wa vitu wanavyozalisha ili waweze kuingia kwenye sokoa au ndio iwe sehemu ya malighafi kwenye viwanda ambavyo vinajengwa na vilivyopo. Labda, kingine ninachosisitiza sana kwa sababu pia tunashirikiana na kwa ukaribu na taasisi ya uwezeshaji ya Taifa (National Economic Empowerment), tunawajengea watu wawe na utajiri zaidi wa kiuchumi, lakini tunasema hawa watu wa chini nao wasisahauriwe kwa sababu wameanzisha vikundi kwenye shughuli zao za kiuchumi. Niseme tu siku zote tunaendana na mipango ya Taifa na kwa sababu Tasaf ipo nchini nzima, ipo kwenye vijiji vyote hatuwezi tukakinzana na sera nyingine yeyote zaidi ya kushirikiana kwa pamoja.

Swali: Mnashirikiana vipi na mamlaka zingine kama halmashauri za wilaya katika kuwapa fursa wanufaika wa Tasaf kushiriki matamasha ya biashara au makongamano katika kutambulisha bidhaa zao na kupata soko?

Jibu: Kama Tasaf huwa tunawaleta walengwa wetu kwenye maonyesho yoyote yawe ya kitaifa, yawe ya eneo maalumu au maonyesho yanayohusisha taasisi za fedha ili wapate fursa kuonyesha kile wanachokifanya na kupata mawazo ya kuboresha. Kwenye ngazi ya halmashauri kwa sababu wanavitambua hivyo vikundi wao wana mfuko wa kuwezesha vijana na wanawake. Sasa katika makundi yetu kule kuna vijana na wanawake na katika kaya maskini tuna vijana na kina mama ambao wana shughuli zao za kiuchumi hivyo ni muhimu nao wakakumbukwa kupewa mikopo inayotolewa kwenye ngazi ya halmashauri.

Swali: Je, mnawabaini vipi watu wasio na sifa ya kuwa wanufaika wa Tasaf na hatua gani zinachukuliwa kwa watakaobainika?

Jibu: Huu mpango muundo wake unashirikisha jamii tangu ngazi ya chini na misingi yake ni mikubwa ya uwazi na uwajibikaji ambapo katika mikutano ya hadhara wanajiwekea vigezo vya kutambua kaya maskini na wanachagua kamati za kulinganisha au kuchambua wale waliotajwa kutoka kaya maskini. Siwezi kukataa kwamba kumekuwapo na changamoto ya viongozi wa ngazi ya chini na wasimamizi ambao sio waaminifu waliweka majina yao kwa lengo la kunufaika, lakini Rais Magufuli aliagiza mwaka jana kufanya uhakiki na tukaifanya hiyo kazi.

Tumefanya uhakiki nchi nzima na waliopo sasa wote ni wenye sifa na wasio na sifa wameondolewa, watu sasa wametambua kwamba kuna ufuatiliaji tena ule wa uwazi ambao hauwezi kuwa na maficho. Pia, kwa kutumia vyombo vya dola hatua za kisheria zimechukuliwa dhidi ya wale waliobainika kufanya udanganyifu.

Mfano, kuna viongozi waliokuwa kwenye serikali za vijiji lakini ni maskini,hapo ndio kulikuwa na changamoto. Wapo kwenye serikali ya vijiji, lakini wakawa wamejiingiza kwenye mpango, sheria haitaki hivyo kwa sababu unaleta mgongano wa masilahi. Hao nao ilibidi watoke, lakini wengine waliona ni vema watoke kwenye serikali ya vijiji ili waweze kuingia kwenye mpango.

Hata hivyo, tunaelewa katika kuondoa umaskini kuna kwenda pamoja na kutambua shida na kero za wananchi na ushirikishwaji, kwa hiyo tulijenga shule, zahanati, barabara za vijijini, miradi ya maji na miradi ya mazingira. Dhana na msingi mkubwa wa kuondoa umaskini ni pamoja na kuboresha huduma za jamii. Zile kaya maskini zilikuwa hazipeleki watoto shule, hazishiriki huduma za afya kwa hiyo wanazidi kuwa maskini, baba hajui kusoma na kuandika na watoto hivyo hivyo na vizazi vijavyo kwa hiyo mpango wa Tasaf awamu ya tatu unalenga kuwezesha na kuongeza matumizi katika kaya ili wapate chakula, lakini pia wapate huduma za msingi kama vile elimu na huduma za afya. Inawezekana ikawepo shule lakini haina walimu au madawati, kazi yetu ni kuondoa hizo kero au inawezekana zahanati ikawepo lakini hakuna nyumba ya daktari au maji kwa utaratibu ule ule ni kazi yetu kuweka maji au kujenga nyumba ya daktari.

Kwa kufanya hivyo itawezesha kaya maskini zilizo kwenye mpango kupata huduma zote muhimu. Mfano, mtoto anayetoka kwenye kaya maskini akiwezeshwa kwenda shule huko akute walimu, madawati na mwanafamilia wa kaya maskini anapougua akienda zahanati akute daktari na huduma zingine muhimu kama maji.

Swali: Kipimo cha waliofanikiwa kuondokana na umaskini ni kipi na utaratibu upi unatumika kuwaondoa kwenye mpango?

Jibu: Kitu cha msingi ni kuwajengea uwezo ili waelewe mpango una malengo gani na kwamba watambue Tasaf haipo siku zote, lakini watambue kwamba mnufaika anakuwapo ndani ya mpango kati ya miaka mitatu hadi mitano, baada ya hapo anatakiwa aondoke kupisha wengine. Hata hivyo, mnufaika aliyefanikiwa kabla ya kutolewa kwenye mpango anaandaliwa kwa kupewa taarifa miezi sita kabla na pia inakuwa shirikishi kama utaratibu ulivyofanyika wakati wa kuingizwa kwenye mpango.

Hivyo, ile miezi sita ya maandalizi ya kutoka mnufaika hupewa ajira kwenye miradi ya kijiji kwa lengo la kumuandaa kujitegemea kwa kufanya shughuli zingine za kiuchumi. Miradi wanayopata ajira ni ile ya kijiji mfano ujenzi wa vyumba vya madarasa au jengo la zahanati. Lakini, baada ya hapo tunawahamasisha kuanzisha vikundi na kuwekeza akiba zitakazowawezesha kukopa mitaji.