Keisha anakomaa na malezi, muziki na siasa

Hadija Shaaban ‘Keisha’


Muktasari:

Kumbe ukimya wake wa kutokutoa nyimbo muda mrefu ulisababishwa na kuwa ‘bize’ kwenye masomo

Dar es salaam. Si mwanamuziki mwenye makuu wala skendo, mtulivu fulani hivi, sauti yake nyororo inavutia kuisikiliza pale anapokuwa anaimba. Ni mwanadada, Hadija Shaaban ‘Keisha’ ambaye amefichua kwa nini alikuwa kimya kwenye anga hizo.

Kumbe ukimya wake wa kutokutoa nyimbo muda mrefu ulisababishwa na kuwa ‘bize’ kwenye masomo ambapo kwa sasa tayari amekwishamaliza shahada ya manunuzi na usambazaji.

Jingine lililomuondoa usoni mwa mashabiki wake kwa muda mrefu nje na masomo aliyoyataja, ni kutingwa na vikao vingi vya majukumu ya kisiasa kwani yeye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.

“Lakini pia ukiachana na mambo mengi ninayoyafanya yanayojulikana machoni pa watu, lakini mimi ni mama wa watoto watatu na mume pia lazima nitenge muda wa kuwa pamoja nao,”anasema.

Amerudi kivingine

Wimbo wake wa mwisho kutamba sokoni ulikuwa ‘Nimechoka’ aliomshirikisha Diamond Platnumz ambapo kwa sasa ujio wake mpya umekuwa kivingine tofauti na alivyozoeleka, ametoa kibao ‘Nioe’.

Anaeleza maudhui ya wimbo huo kuwa ni maalumu kwa wanawake wote ambao wako kwenye uhusiano kwa muda mrefu, anawakumbusha wawaombe wanaume wao wawaoe na kuachana kisela.

“Wanawake lazima ifikie hatua ya kuwashawishi wanaume zao kufunga nao ndoa, unakuta kuna mtu amekaa na mtu zaidi ya miaka 10, sasa hapo anakuwa anasubiri nini,” anahoji.

Anavyoliona gemu

Anakiri mambo kwa sasa si shwari kama ilivyokuwa zamani na kwamba, mwenye uwezo mzuri wa mashairi na kuimba ndiye aliyekuwa anapata nafasi sokoni.

Anaeleza kuwa kwa sasa kwamba mambo yote yamehamia kwenye mitandao kwa asilimia kubwa.

“Kwa sasa hata kama una wimbo mkali bila kuwa na watu wengi ambao wanakufuatilia kwenye mitandao ya kijamii inakuwa ngumu kufika mbali, kwani asilimia kubwa wengi wanatumia kiki ambazo zinafanya kazi zao zivume ingawa haziishi ambazo nazo zinapitia katika mitandao hiyohiyo,” anasema.

Nandy anavuma, Ruby mkali wa sauti

Pamoja na kimya kingi, alikuwa mfuatiliaji mzuri wa kile wanachofanya Nandy aliyemuelezea kwamba anavuma, huku Ruby akikiri kwamba ni mtaalamu wa kucheza na sauti.

“Kusema ukweli Nandy ndiye anavuma kwa sasa, ila ukizungumzia mtaalamu ama anayeweza kucheza na sauti basi Ruby yupo vizuri sana,” anasema.

Hataki watoto wake wafanye muziki

Keisha hataki kabisa watoto wake waje kujihusisha na muziki, akitaja sababu kubwa kwamba wanaweza wakawa na mapokeo potofu yanayoweza kuwagharimu.

“Nimeolewa, nimefanikiwa kupata watoto watatu, ninachohofia vijana wangu wasijihusishe na muziki wanaweza wakaingia kwenye gemu kwa ulimbukeni, tofauti na mimi ambaye nimefuata kazi, ndiyo maana huwezi kunisikia na kashfa yoyote,” anasema.

Kuhusu Basata

Ukiachana na Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), kutoa taratibu mpya ambazo zinatakiwa kufuatwa na wasanii mbalimbali zikiwamo kampuni kutakiwa kulipa ada ya kiasi cha Sh5 milioni kwa kila msanii ambaye wanamtumia katika kazi zao, ambapo ni utaratibu ambao huko nyuma haukuwepo hali iliyosababisha wasanii kadhaa kuikosoa, yeye anaona tofauti.

Kwa Keisha, anasema haoni tatizo kwa sababu ni taratibu ambazo zimewekwa, hivyo zinahitaji kufuatwa kwa kuwa ndizo zinazowaongoza wasanii.

“Nimesikia pia Diamond alizuiliwa, nadhani zote ni taratibu kama vile sehemu yoyote unaweza kuwekewa na hivyo inabidi kuzifuata kwa sababu ndizo zinazotupa muongozo sisi wasanii.

“Basata ipo chini ya Wizara ya Habari na Utamaduni na Michezo, hivyo ni kitu cha kawaida kwa jinsi wanavyofanya sababu ndiyo kazi ambazo inatakiwa wazifanye kuhakikisha sanaa inaenda katika mstari mzuri, kwangu sioni tatizo,” anasema.

Je, siasa kwake inampa tafu kwenye muziki? Akiwa kama mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, anasema inamsaidia pia katika kazi zake za sanaa.

“Yaani napewa sapoti sana na wanachama wenzangu na pia wao ndiyo walikuwa mstari wa mbele wakiniomba sana nirudi kwenye muziki na sasa nina imani huko waliko wanafurahi sana, maua nimerudi kama hivi,” anasema.

Kiki katika muziki

Muziki wa Bongo kwa sasa umekuwa ukitawaliwa na kiki za wasanii mara kwa mara, lakini kwake Keisha anasema haoni haja kwa wasanii kufanya hivyo kwa sababu haina sapoti kubwa kwa muziki wao na nafasi zao siku za baadaye.

“Sasa mfano unafanya muziki leo na kiki yako hiyo vipi ikiisha? Na wimbo wako nao unapotea, kwa hiyo utafanya kiki mpaka lini? Cha msingi nawashauri tu hasa wanamuziki wa kike wafanye muziki mzuri kama sisi zamani kazi yako nzuri ndiyo iliyokuwa inakupa jina na thamani kubwa.

“Mimi sijawahi kufanya kiki yoyote na sitegemei kabisa kuja kufanya hayo kwa sababu naamini mashabiki wa Keisha wanapenda sauti yangu na utunzi wangu, hayo mengine nitawaudhi tu,” anasema.