Kenya waichangamkia Jamii Forums

Mkurugenzi na mwanzilishi wa mtandao wa Jamii Forums, Maxence Melo


Muktasari:

Juni 11, Jamii Forums ilisitisha huduma zake kutokana na tangazo lililotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Dar es Salaam. Siku chache baada ya mtandao wa Jamii Forums kusitisha huduma zake, umebainika unafanya kazi kwenye mtandao maarufu wa Kenya Talk wa nchini Kenya.

Juni 11, Jamii Forums ilisitisha huduma zake kutokana na tangazo lililotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Juni 10, TCRA ilitoa notisi ikielekeza kuwa ni kosa kisheria kutoa na kuchapisha taarifa kwa njia ya mtandao bila kuwa na leseni ikitoa hadi Juni 15 kutekelezwa kwa sharti hilo.

Hata hivyo, akizungumza kwa simu na Mwananchi, mkurugenzi na mwanzilishi wa mtandao huo, Maxence Melo alikanusha kuihamishia Jamii Forums nchini Kenya, akisema hawana makubaliano na waliouhamisha.

“Hatujahamishia Jamii Forums Kenya, hao wanaoendesha jukwaa hilo inawezekana wameona Tanzania imezuia sauti za watu kwa hiyo wamezichukua wao. Kama sauti zetu zinazuiwa, wengine wanachukua wanaendelea,” alisema Melo.

Huku akitoa mfano wa wafanyabiashara, Melo alisema nchi za jirani zinatumia matatizo yanayotokea Tanzania kujinufaisha.

“Kwa mfano kuna wakati wafanyabiashara walikuwa wanalalamikia mazingira mabovu ya biashara, hawakusikilizwa, wakaamua kwenda Kenya kuwekeza hisa zao,” alisema Melo.

Alisema tangu walipoamua kusitisha huduma zao , wamefanya jitihada za kuzungumza na TCRA bila mafanikio hata hivyo alisema wataendelea kuwatafuta ili kupata suluhisho.

Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa Jamii Forums inapatikana katika mtandao wa Kenya Talk. Katika ukurasa wa Kenya Talk wa yaliyomo kuna orodha ya majukwaa mbalimbali ikiwemo Jamii Forums.

Ndani ya Jamii kuna majukwaa yaleyale yaliyokuwemo ikiwamo Jukwaa la Siasa, Jamii Intelligence, habari mchanganyiko, biashara, uchumi na ujasiriamali, mahusiano, mapenzi na urafiki, international forum, utani, michezo na burudani.

Katika jukwaa la siasa, miongoni mwa mada zilizotumwa ni pamoja na ‘hivi malaika waliosemwa hapa ni akina nani?’ ambayo wachangiaji mbalimbali wanaojitambulisha kuwa Watanzania wameendelea kuchangia.

Mchangiaji mmoja anayejitambulisha kama ‘Sijuti’ ameweka nukuu ya Rais John Magufuli aliposema : “Nilikuwa natamani siku moja malaika washuke waizime hii mitandao yote, ili baada ya mwaka mzima itakapokuja kufunguka wakute sisi tumeshatengeneza Tanzania yetu mpya.”

Hivi karibuni viongozi wa Jamii Forums walioshitakiwa akiwemo Melo wameshinda kesi moja kati ya tatu zilizofunguliwa na Serikali.

“Tumeshinda kesi moja kati ya tatu zilizokuwepo. Nadhani baada ya kuona wameelemewa mahakamani ndiyo wameamua kutufungia. Inawezekanaje mamlaka inayokusimamia ndiyo hiyo hiyo inayotunga kanuni za kukushitaki?” alihoji Melo.