Serikali yamfukuza kiongozi wa upinzani Kenya

Muktasari:

Serikali imeandika kuwa Wizara ya Ulinzi ilitii agizo hilo na kumpatia tiketi ya kwenda nyumbani kwake Canada ambapo ana uraia wa nchi hiyo alioupata Juni 16, 2017.


Nairobi. Serikali ya Kenya imemfukuza kwa nguvu na kumsafirisha kwenda nchini Canada mmoja wa viongozi wa upinzani Kenya, Miguna Miguna usiku wa kuamkia leo Februari 8 baada ya mahakama kudai aachiwe huru.

Katika akaunti ya Twitter ya Serikali inayofahamika kwa jina la ‘Nexus’ iliandika katika ukurasa huo Februari, 6 saa 7:19 usiku kuwa Miguna anaelekea nyumbani Canada baada ya mahakama kuamuru aachiwe.

Serikali imeandika kuwa Wizara ya Ulinzi ilitii agizo hilo na kumpatia tiketi ya kwenda nyumbani kwake Canada ambapo ana uraia wa nchi hiyo alioupata Juni 16, 2017.

“Miguna ameelekea nyumbani. Mahamakma iliamuru aachiwe na Wizara ya Ulinzi imetii amri na imempatia tiketi ya kwenda nyumbani. Tafadhali tunasisitiza alipatiwa kibali cha kuishi Canada Juni, 16 2017” umeandika ukurasa huo.

Miguna amesafirishwa na Shirika la Ndege la KLM ambalo lilipoulizwa na wananchi katika ukurasa wao wa Twitter unaofahamika kwa jina la ‘Royal Dutch Airline’ walipendekeza maswali yote waulizwe mamlaka husika kwa sababu za kiusalama.

Miguna alishikiliwa na Polisi Februari, 2 kwa tuhuma za kushiriki kuapishwa kwa Raila Odinga kama Rais wa watu wa Kenya Januari, 30.

Mwanasheria wa Miguna, Dk John Khaminwa amesema mteja wake kwasasa hayupo nchini humo.

“Ni kweli. Ameondolewa kwa nguvuy na ndege ya KLM na tunasikia ameelekea Canada. Ni uvunjaji wa haki” amesema Khaminwa.

Kuhusu sakata la uraia wake, Dk Khaminwa amesema Miguna aliukana uraia wa Kenya ila miezi miwili kabla ya uchaguzi mkuu aliomba tena.

“Miguna alipokamatwa Serikali ya Canada iliiandikia barua Kenya kuelezea kuwa mwananchi wao ananyanyaswa,” amesema Khaminwa.

Katika kipande kifupi cha video kinachosambaa mtandaoni kimemuonyesha kiongozi huyo akiwa katika ndege na amevalia suti, barakashia akiwa peke yake siti za mbele.