Kenyatta amlilia Kenneth Matiba

Muktasari:

Mwanasiasa huyo mkongwe aliyefariki jana jioni ndiye mwanzilishi wa vuguvugu la mikutano ya Sabasaba ya mwaka 1990 na 1997.

 Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametuma salamu za rambirambi  kupitia ukurasa wake wa Twitter kuhusu kifo cha aliyewahi kuwa mgombea urais nchini humo, Kenneth Matiba.

Mwanasiasa huyo mkongwe aliyefariki jana jioni ndiye mwanzilishi wa vuguvugu la mikutano ya Sabasaba ya mwaka 1990 na 1997.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Rais wa Kenya Rais  Kenyatta aliandika, “Ni kwa moyo mzito na wenye simanzi, mimi na Margaret (mke wangu) tunatuma salamu zetu za rambirambi kwa Edith Matiba (mke wa marehemu) baada ya kifo cha Mzee Kenneth Matiba.”

Pia Makamu Rais, William Ruto amesema Taifa limepoteza mtu mkubwa sana.

“Tumetandwa na majonzi, tunatoa heshima kwa Kenneth Matiba kwa kupigania demokrasia, haki za binadamu na mpiganiaji wa wanyonge,” amesema.

Matiba ambaye ni maarufu katika siasa za ‘ukombozi wa pili wa kisiasa’ nchini humo baada ya ile ya Uhuru miaka ya 1950 na 1960.

Mwanasiasa huyo maarufu ambaye alitatizwa pa kubwa kisiasa na Rais wa awamu ya pili nchini humo, Daniel Toroitich Arap Moi alizaliwa Juni mosi mwaka 1932 Wilaya Muranga iliyopo katikati mwa Kenya.

Alikuwa mwanasiasa ambaye daima alikuwa akitabasamu na mkereketwa wa kutetea haki za kibinadamu na kuwepo kwa demokrasia nchini humo.

Aliwahi kuwania kiti cha urais mwaka wa 1992, lakini akaibuka wa pili nyuma ya Moi.

Pia, amewahi kuwa mwenyekiti wa halmashauri kuu ya shirika la ndege nchini humo na mwenyekiti wa Shirikisho la Kandanda nchini Kenya (KFF).

Pia ndiye mwasisi na mwenyekiti wa Kenya Football League, mwenyekiti wa chama tawala wakati huo cha  Kanu wa tawi la Mbiri na naibu mwenyekiti wa Kanu tawi la Wilaya ya Murang'a.

Matiba ambaye ni mfanyabaishara  maarufu, alikuwa mwana kamati wa kitaifa wa shirika la wamiliki wa hoteli nchini humo na mmiliki wa gazeti maarufu la upinzani la The People. Matiba alifariki saa 12:10 jana Jumapili.