Kero tatu za Muungano bado hazijatatuliwa

Muktasari:

Amesema miongoni mwa kero hizo ni ile ya Tume ya pamoja ya fedha ambayo inahusu makato na gharama za kuchangia shughuli za Muungano.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, amesema kero za Muungano tatu kati ya 15 bado hazijatatuliwa.

Amesema miongoni mwa kero hizo ni ile ya Tume ya pamoja ya fedha ambayo inahusu makato na gharama za kuchangia shughuli za Muungano.

January na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi na Ajira, Jenista Mhagama na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana jana walikuwa wakizungumzia maandalizi ya maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano, yaliyofanyika mjini hapa.

January alizitaja kero nyingine zinazoendelea kushughulikiwa kuwa ni usajili wa vyombo vya moto ambayo utatuzi wake utapatikana katika marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani.

Alisema marekebisho ya sheria hiyo yapo katika maandalizi na waraka wake upo. “Kero nyingine ni la hisa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki ambayo nayo inaendelea kushughulikiwa,” alisema January.

Alisema kamati ya pamoja ya Serikali ya Muungano ya Tanzania chini ya uongozi wa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), itakaa mwaka huu kupokea taarifa ya kushughulikiwa kero hizo.

“Nchi nyingi duniani zimefeli katika mambo ya Muungano kwa sababu hazina mfumo thabiti wa kushughulikia masuala ya hayo Muungano,” alisema Makamba.

Mhagama alisema sherehe hizo ambazo mgeni rasmi atakuwa Rais, John Magufuli, zitaanza saa moja asubuhi na kumalizika saa sita.

Alisema pia kutakuwa na gwaride la heshima lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Jeshi la Polisi na Magereza sambamba na maonyesho ya kikosi cha makomandoo.

Mkuu wa Mkoa, Rugimbana aliwataka wakazi wa Dodoma na viunga vyake, kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maadhimisho hayo na kwamba, milango ya kuingia Uwanja wa Jamhuri itafunguliwa saa 12:00 asubuhi na kufungwa saa 1:30 asubuhi.

Mizinga itapigwa ambayo ni salama ila tunawashauri wale wanaoishi maeneo ya karibu na uwanja kuacha madirisha wazi,” alisema.

“Kutakuwa na onyesho la ukakamavu na uzalendo la wanafunzi kutoka shule za sekondari mkoa wa Dodoma na vikundi vya burudani vya ngoma za asili kutoka Dodoma na Zanzibar,” alisema.

Alisema kutakuwa pia na burudani ya bendi ya muziki wa kizazi kutoka Dodoma (Mchungaji Zayumba, Jaco Beats na Mgosi matarumbeta) na kutoka Dar es Salaam itakuwapo Yamoto Band na Mwenge Jazz.

w