Kesi kupinga kuondolewa chaneli za ndani katika ving’amuzi yafunguliwa

Muktasari:

  • Jaji anayeisikiliza aiahirisha hadi kesho

Iringa. Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imeahirisha kupokea maombi ya kesi ya kupinga kuondolewa kwa chaneli za ndani kwenye ving’amuzi vya Azam, Dstv, Zuku na Star times iliyofunguliwa mahakamani hapo na watu watano hadi kesho.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania anayesikiliza kesi hiyo, Penterine Kente leo Septemba 3, 2018 amelazimika kuahirisha shauri hilo kwa dakika 20.

Uamuzi huo aliufanya baada ya kutokea ubishani wa kisheria baina ya mawakili wa upande wa waleta maombi na wakili wa Serikali aliyetaka mahakama kutoa muda mpaka walalamikiwa wengine watakapokuwepo mahakamani jambo lililopingwa na mawakili wa upande wa waleta maombi.

Baada ya mabishano hayo Jaji Kente aliamua kutoa muda wa dakika 20 ili kila upande ukaweke vizuri hoja zao na waliporejea baada ya muda huo Jaji aliamua kuahirisha kesi hiyo mpaka leo.

Katika kesi hiyo waleta maombi Silvanus Kigomba, Jesca Msambatavangu, Oliver Motto, Sebastian Emmanuel Atilio na Hamdun Abdallah wanaiomba mahakama kubatilisha amri ya kuondolewa chaneli za ndani kwenye ving’amuzi vya kampuni hizo.

Wanasema ving’amuzi hivyo ambavyo wamekwishavitumia kwa muda mrefu na wananchi wamevinunua baada ya kuamini watapata huduma ya kutazama maudhui yanayorushwa na chaneli za ndani kupitia ving’amuzi hivyo.

Katika kesi hiyo namba moja ya mwaka 2018 waleta maombi wanawakilishwa na mawakili wawili Chance Luwoga na Edmond Mkwata.

Edmond amewataja walalamikiwa ni pamoja Multichoice (T) Limited, Simba net (T) Limited, Azam Televison, Starmedia (T) LTD, Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Mwanasheria MKuu wa Serikali.

Akizungumza kwa niaba ya walalalamikaji hao, Msambatavangu amesema kimsingi wao ni walaji wa habari na walikuwa wanapata habari kupitia chaneli za Tanzania za ndani ya nchi kwa hiyo kutokana na malumbano ya watoa huduma na serikali kwa sasa hawapati huduma hizo.