Kesi ya Barlow Aprili 27

Marehemu Liberatus Barlow enzi za uhai wake

Muktasari:

  • Mara ya mwisho shauri hilo namba 192 la mwaka 2016, linalowakabili washtakiwa Michael Muganyizi, Chacha Waikane, Magige Mwita, Buganzi Edward, Bhoke Marwa, Abdallah Petro na Abdulrahman Ismail, liliahirishwa Machi 24 mwaka jana.

Mwanza. Kesi ya mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow itaanza kusikilizwa mfululizo kuanzia Aprili 27 hadi Mei 8 katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza.

Mara ya mwisho shauri hilo namba 192 la mwaka 2016, linalowakabili washtakiwa Michael Muganyizi, Chacha Waikane, Magige Mwita, Buganzi Edward, Bhoke Marwa, Abdallah Petro na Abdulrahman Ismail, liliahirishwa Machi 24 mwaka jana.

Kabla ya kuahirishwa, Mahakama Kuu ilikuwa imesikiliza ushahidi kutoka kwa mashahidi 12 kati ya 36, wanaotarajiwa kuitwa na upande wa Jamhuri.

Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Francis Kabwe alisema kusikilizwa kwa shauri hilo kunatokana na Mahakama kupata fedha za kugharamia uendeshaji.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kabwe alisema shauri hilo litasikilizwa mbele ya Jaji Sirilius Matupa. Barlow aliuawa kwa kupigwa risasi Oktoba 12, 2012 katika tukio lililotokea eneo la Kitangiri wilayani Ilemela.