Mashahidi wakwamisha kesi ya Bilionea Msuya

Muktasari:

Washtakiwa walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza mwaka 2013.

Upande wa Mashitaka katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Erasto Msuya umesababisha kesi kuahirishwa kutokana na kutokuwepo shahidi.

Kesi hiyo ilipangwa kuendelea kusikilizwa leo Februari 23,2018 kwa kuwasilisha ushahidi wa shahidi wa 26 wa upande wa mashitaka.

Hata hivyo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula aliiarifu Mahakama kuwa hapakuwa na shahidi.

Mbele ya Jaji Salma Maghimbi, Wakili Chavula aliiomba Mahakama kuiahirisha kesi hiyo hadi atakapopatikana shahidi.

Hadi Februari 21, upande wa mashtaka ulikuwa umeita mashahidi 25 waliotoa ushahidi akiwemo mtaalamu wa kemia na uchunguzi wa sayansi ya jinai, Gloria Omari.

Jaji wa Mahakama Kuu, Salma anayesikiliza kesi hiyo aliridhia ombi hilo na kuahirisha kesi hadi itakapopangwa katika kikao kingine cha Mahakama.

Awali, kesi hiyo ilipangwa kuendelea kusikilizwa mfululizo hadi Februari 28, mwaka huu.

Washtakiwa saba walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza mwaka 2013 na wanaendelea kushikiliwa mahabusu.