Kesi ya Scorpion yapigwa kalenda

Muktasari:

Kesi hiyo iliyopo katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, imeshindwa kuendelea kutokana na shahidi namba nane katika kesi hiyo, Deus Magosa (45) maarufu Pamba D, kushindwa kufika mahakamani ikielezwa anaumwa kisukari na shinikizo la damu.

Dar es Salaam. Kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi inayomkabili Salum Njwete (34) maarufu Scorpion, imeshindwa kuendelea kutokana na shahidi kushindwa kufika mahakamani kutokana na kuumwa.

Kesi hiyo iliyopo katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, imeshindwa kuendelea kutokana na shahidi namba nane katika kesi hiyo, Deus Magosa (45) maarufu Pamba D, kushindwa kufika mahakamani ikielezwa anaumwa kisukari na shinikizo la damu.

Magosa ambaye ni kamanda wa ulinzi shirikishi katika eneo la Buguruni, alitakiwa kutoa ushahidi jana. Wakili wa Serikali, Chesesi Gavyola aliieleza Mahakama na kuiomba ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Hakimu, Flora Haule anayesikiliza shauri hilo, alikubali ombi hilo na kuahirisha kesi hadi Mei 2.

Njwete anadaiwa kutenda kosa la wizi na kujeruhi Septemba 6, mwaka jana eneo la Buguruni Sheli. Katika shtaka la kwanza, anadaiwa kuiba mkufu wa madini ya fedha wenye uzito wa gramu 34 na thamani ya Sh60,000; bangili yenye thamani ya Sh85,000, pochi na fedha taslimu Sh331,000.

Vitu hivyo vinadaiwa kuwa na thamani ya Sh476,000 mali ya Saidi Mrisho.

Katika shtaka la pili, anadaiwa kabla na baada ya wizi huo, alimjeruhi kwa kumchoma kisu Mrisho machoni, begani na tumboni ili kujipatia mali hizo.