Kesi ya kina Mbowe, vigogo Chadema yakwama kusikilizwa

Viongozi wa Chadema wakimsikiliza mwanasheria wao, Peter Kibatala (kulia) wakiwa kizimbani baada ya kusomewa maelezo ya awali ya kesi yao ya jinai katika Mahakama ya Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 27, 2018

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuwasomea maelezo ya awali mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na vigogo wengine wanane wa chama hicho kutokana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji kutokuwepo mahakamani.

Wakili wa utetezi Peter Kibatala alieleza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri leo Jumatatu Juni 25, 2018 kuwa Dk Mashinji hayupo mahakamani amekwenda Songea katika kesi nyingine ya jinai inayomkabili ya mwaka 2017 na kwamba katibu mkuu huyo ni mshtakiwa namba moja katika kesi hiyo.

Mbowe ambaye hivi karibuni alifiwa na kaka yake alikuwepo mahakamani hapo pamoja na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko ambaye mahakama hiyo ilimtaka leo awepo mahakamani baada ya awali kuripotiwa kuwa alikuwa mgonjwa.

Kibatala ameieleza mahakama kuwa Matiko bado ni mgonjwa na amekuja kutokana na amri ya mahakama iliyomtaka ahudhurie bila kukosa kwa kuwa ilielezwa asipofanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Washtakiwa wengine waliokuwepo mahakamani ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar); mbunge wa Kibamba, John Mnyika;  mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche;  Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na  mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Wakati Kibatala akiomba kesi hiyo iahirishwe hadi Juni 29, 2018, wakili wa upande wa mashtaka Paul Kadushi aliomba iendelee kusikilizwa kesho.

Baada ya maelezo ya mawakili hao, hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 27, 2018 ili kutoa nafasi kwa Dk Mashinji kurejea kutoka Songea na kuungana na wenzake kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali na kusikilizwa mfululizo hadi Juni 29, 2018.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa 13.