Kesi ya kina Mbowe kusikilizwa kwa siku tano mfululizo

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  itawasomea maelezo ya awali (PH) na kuanza rasmi kuisikiliza kesi ya jinai inayowakabili viongozi tisa wa Chadema akiwamo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwa siku tano mfululizo, kuanzia Juni 25 hadi 29, 2018.

 

Mbowe na wenzake walipaswa kusomewa maelezo ya awali leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri lakini ilishindikana  kwa sababu mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Freeman  Mbowe amefiwa na kaka yake Henry Mbowe na amekwenda msibani, Moshi.

 

Pia, Mahakama imemtaka mshtakiwa wa tano katika kesi hiyo, Esther Matiko mbunge wa Tarime mjini ambaye ni mgonjwa ahudhurie mahakamani bila ya kukosa na  asipofanya hivyo hatua dhidi yake zitachukuliwa.

 

Hata hivyo, mawakili wanaowatetea washtakiwa hao Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya hawakuwapo mahakamani, Kibatala alikuwa amehudhuria kesi  Mahakama Kuu, huku Mtobesy, akihudhuria kesi Mahakama ya Afrika Mashariki  Arusha.

 

Hivyo waliwakilishwa mahakamani hapo na mawakili Nashon Nkungu, Frederick Kihwelo na Hekima Mwesigwa.

 

Awali,  wakili wa  Serikali Mkuu,  Faraja Nchimbi   alieleza mbele ya Hakimu  Mashauri kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa Maelezo ya awali na  kwamba wamejipanga kuendelea.

 

Lakini ilishindikana kwa sababu Mshtakiwa 

Mbowe hakuwapo mahakamani  kwa sababu amefiwa na kaka yake Henry Mbowe na amekwenda Moshi katika mazishi.  

 

Mbowe aliwakilishwa mahakamani hapo na mdhamini wake Grayson Celestine ambaye aliwasilisha nakala ya cheti cha kifo mahakamani ili kuithibitishia Mahakama.

 

Kwa upande wa mshtakiwa Esther Matiko aliwakilishwa na mdhamini wake, Patrick John aliyeieleza Mahakama kuwa anaumwa na akawasilisha nyaraka ya mapumziko kutoka kituo cha afya.

Hata hivyo, nyaraka hiyo ilipingwa na wakili Nchimbi kwa madai kuwa ni batili haina Maelezo yanayojitosheleza ambayo yanayoweza kuishawishi mahakama kuamini Matiko ni mgonjwa na anapaswa kupumzika kwa siku saba.

 

Washtakiwa waliokuwapo mahakamani ni mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu Bara na John Mnyika.

 

Katibu wa chama hicho, Dk Vicenti Mashinji, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.

 

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwamo kufanya mkusanyiko usio halali, na kusababisha ghasia. Pia wanadaiwa Februari mwaka huu walikiuka agizo la kuwataka kutawanyika na kusababisha uvunjifu wa amani.