Kesi ya mauaji ya mwanafunzi kusikilizwa Agosti 27

Muktasari:

  • Kesi hiyo inamkabili mmiliki wa shule hiyo, Edward Shayo, mkuu wa shule, Labani Nabiswa na mlinzi, Hamis Chacha.

Moshi. Usikilizwaji wa awali wa kesi ya mauaji ya kukusudia ya mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Scolastica iliyopo mji wa Himo, Humphrey Makundi umepangwa kufanyika Agosti 27.

Kesi hiyo inamkabili mmiliki wa shule hiyo, Edward Shayo, mkuu wa shule, Labani Nabiswa na mlinzi, Hamis Chacha.

Mwanafunzi huyo alitoweka shuleni Novemba 6, 2017 na baadaye kubainika ameuawa.

Mwili wa mtoto huo uliokotwa Novemba 7, katika Mto Ghona mita zipatazo 300 kutoka shuleni na polisi waliouchukua waliupeleka Hospitali ya Mawenzi na kuzikwa kwa madai haukutambuliwa.

Usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo umepangwa kufanyika mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Moshi, Aishiel Sumari Agosti 27 mjini Moshi.

Ratiba ya kikao cha Mahakama Kuu kilichoanza Agosti 13 na kutarajiwa kumalizika Agosti 28 iliyosambazwa kwa mawakili wa utetezi inaonyesha washtakiwa wanatetewa na wakili Elikunda Kipoko. Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa Agosti 10, usikilizaji wa awali utahusisha pia kesi za kusafirisha dawa za kulevya.

Ingawa naibu msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Frank Mahimbali aliyeandika barua hiyo hakupatikana, lakini Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), kimethibitisha kuanza kwa kikao hicho.

Mwenyekiti wa TLS mkoani Kilimanjaro, David Shillatu akizungumza na Mwananchi alisema katika hatua hiyo, watakaokiri makosa watahukumiwa na watakaokana kesi zao zitaenda hatua ya usikilizwaji.

Usikilizwaji wa kesi ya Shayo na wenzake unafanyika kukiwa na madai ya baadhi ya ushahidi muhimu kutokuwapo kwenye jalada wakati wa kusomwa kwa ushahidi (committal) Agosti 3.

Ushahidi ambao haukuwapo kwenye jalada la waendesha mashitaka ni taarifa ya mawasiliano ya simu usiku wa siku ya mauaji kati ya washtakiwa hao watatu.

Baadhi ya ndugu wa marehemu wanadai kuna vielelezo vya nyaraka havikuwapo kwenye jalada, hivyo wanadhani si vyema kwenda hatua ya pili kabla ya kurekebisha upungufu.

Kaimu mwanasheria mkuu wa Serikali Kanda ya Moshi, Abdallah Chavulla alinukuliwa wiki iliyopita akisema ingawa yeye si msemaji wa suala hilo lakini madai hayo yana lengo la kuchafua watu.

Chavulla alinukuliwa akisema kinachokwenda mahakamani kuthibitisha shtaka ni kile ambacho mwendesha mashtaka anaona kinafaa na kinaweza kujenga hoja katika ushahidi na siyo vinginevyo.