Kesi ya mke wa Bilionea Msuya yapigwa kalenda tena

Muktasari:

Hayo yalitokea leo muda mfupi baada ya Wakili wa Serikali, Kishenyi Mutalemwa kuieleza mahakama kuwa kesi ingesomwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi lakini Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa anayeisikiliza kesi hiyo alisema hawezi kutoa uamzi kwa sababu kuna barua toka kwa ndugu wa Msuya  na anasubiri maelekezo.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imeshindwa kutoa uamuzi katika kesi ya mauaji inayomkabili mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na Revocatus Muyela na kuiahirisha hadi Februari 6, 2017.

Hayo yalitokea leo muda mfupi baada ya Wakili wa Serikali, Kishenyi Mutalemwa kuieleza mahakama kuwa kesi ingesomwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi lakini Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa anayeisikiliza kesi hiyo alisema hawezi kutoa uamzi kwa sababu kuna barua toka kwa ndugu wa Msuya  na anasubiri maelekezo.

Hakimu Mwambapa alitakiwa atoe uamuzi juu ya hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi  pamoja na upande wa mashtaka ambapo Wakili John Malya aliomba washtakiwa hao waachiwe huru kwa sababu   hakuna hati ya mashtaka inayowashikilia washtakiwa hao mahakama hapo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa yeye aliiomba mahakama iwape muda ili waweze kutekeleza amri ya mahakama iliyotolewa Januari 9, 2017.

 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliamuru washtakiwa hao wa  kesi hiyo ya mauaji ya Aneth Msuya wapewe PF3 ndani ya siku mbili, wakatibiwe baada ya kukubaliana na madai yao, kuwa walipigwa wakati wakiwa mahabusu katika kituo cha Polisi na kwamba hati ya mashtaka inayowakabili mahakamani hapo ni mbovu hivyo ifanyiwe marekebisho.