Kesi ya vigogo Maliasili kuanza Machi

Muktasari:

Vigogo hao wanakabiliwa na mashitaka sita ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka na kuitia Serikali hasara.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Machi 14, mwaka huu kuanza kusikiliza kesi ya matumizi mabaya ya  madaraka, inayomkabili Ofisa Wanyamapori  kutoka Wizara ya Maliasili na Utali, Rajabu Hochi na wenzake wawili.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Ofisa Wanyamapori Mwandamizi kutoka wizara hiyo, Mohamed Madehele na Isaac Maji ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya Uwindaji ya Hunting Enterprises (Tanzania).

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita, likiwemo la matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya dola za Kimarekani 32,599.

Uamuzi huo umetolewa leo Februari 19  na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, baada ya upande wa mashtaka kuwasomea washtakiwa hao hoja za awali(PH).

Awali, akisoma hoja za awali ( PH), wakili kutoka Takukuru Leornad Swai akisaidiana na Pendo Temu, alidai Hochi na Madehele wanakabiliwa na mashtaka matano ambayo ni matumizi mabaya ya madaraka, wakiwa watumishi, Wizara ya Maliasili na Utali.

Hochi na Madehele wamekana kuwa kati ya Januari 12 na Desemba 31, 2008, makao makuu ya wizara hiyo, wakiwa watumishi wa wizara hiyo, wakiwa na wajibu wa kukusanya mapato yanayotokana na uwindaji walishindwa kukusanya kodi na kuipatia faida, Kampuni ya Uwindaji ya Northern Hunting Enterprises (Tanzania) ya dola za kimarekani 250.

Pia Hochi na Madehele wamekana kuwa, kati ya Agosti 11 na Desemba 31, 2011, makao makuu ya wizara hiyo, wakiwa watumishi wa wizara hiyo Kitengo cha Wanyamapori endelevu, wakiwa na jukumu la kukusanya mapato ya uwindaji ya dola 250 kutoka Kampuni hiyo ya uwindaji, walikiuka kanuni na kuinufaisha kampuni hiyo kupata manufaa ya dola za kimarekani 250.

Katika shtaka la tatu, Hochi na Madehele, wamekana kuwa kati ya Septemba 5 na Desemba 31, 2010, makao makuu ya wizara hiyo, wakiwa na jukumu la kukusanya mapato, walishindwa kukusanya faini ya Dola za kimareani 15,630 kutoka Kampuni ya Uwindaji ya Northern Hunting Enterprises (Tanzania), baada ya kuongeza idadi ya uwindaji katika eneo la Hifadhi ya Longido.

 

Katika shtaka la nne, Hochi na Madehele, wamekana kuwa kati ya Septemba 5 na Desemba 31, 2011, wakiwa watumishi wa wizara hiyo, walishindwa kukusanya faini ya dola za kimarekani 250 kutoka katika kampuni hiyo baada ya kuzidisha idadi ya uwindaji wanyamapori katika eneo la Hifadhi ya Longido.

 

Katika shtaka la tano, Hochi na Madehele walikana kuwa kati ya Oktoba 12, 2008 na Desemba 31, 2011 makao makuu ya wizara hiyo, wakiwa na jukumu la kukusanya mapato walishindwa kukusanya faini na kuisaidia kampuni hiyo ya uwindaji, manufaa ya dola za kimarekani 16,219.

 

Katika shtaka la sita, Hochi, Madehele na Maji walikana kuisababishia hasara Serikali ya Dola za kimarekani 32,599, kati ya Oktoba 12, 2008 na Desemba 31, 2011, makao makuu ya wizara hiyo.

Ilidaiwa kuwa mwaka 2008 hadi 2011, wizara hiyo ilitoa kibali cha kuwinda wanyama katika msimu wa uwindaji kwa kampuni ya Northern Hunting Enterprises (Tanzania), katika eneo la Hifadhi ya Longido.

Swai amedai mwaka 2008, kampuni hiyo iliruhusiwa kuwinda digidigi watatu lakini wao waliwinda watano kinyume cha sheria na mwaka 2011, wizara iliruhusu kampuni hiyo kuwinda digidigi wanne lakini wao waliwinda watano, pundamilia sita, ndege na wanyama wengine, wakati wakijua kuwa ni kinyume cha sheria.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, washtakiwa hao walikubali maelezo yao binafsi, kukamatwa kwao, kufikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka yao, lakini wamekana mashtaka sita yanayowakabili.

Hata hivyo washtakiwa hao wapo nje kwa dhamana na kwamba hawaruhusiwi kusafiri nje ya nchi bila kibali cha mahakama na hakimu  Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 14, mwaka huu.