Kesi za kikatiba kuanza kusikilizwa Ijumaa

Dk Makongoro Mahanga 

Muktasari:

  • Mashauri hayo ya kikatiba  yamefunguliwa Mahakama Kuu na umoja wa wanaharakati wa kudai demokrasia Tanzania kwa kushirikiana na wanasheria kupinga namna demokrasia ya vyama vingi, uhuru wa kujieleza na kukusanyika unavyokiukwa hapa nchini. 

Dar es Salaam. Mashauri mawili ya kikatiba yaliyofunguliwa na umoja wa wanaharakati wa kudai  demokrasia Tanzania yataanza kusikilizwa Ijumaa Machi 9, 2018 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Mashauri hayo ya kikatiba  yalifunguliwa katika mahakama hiyo na umoja huo kwa kushirikiana na wanasheria kupinga namna demokrasia ya vyama vingi, uhuru wa kujieleza na kukusanyika unavyokiukwa hapa nchini.

Pia mashauri hayo yalilenga kuhoji namna utendaji wa vyombo vilivyoundwa kwa mamlaka ya kikatiba vinavyoikiuka katiba hiyo.

Mratibu wa Umoja huo Dk Makongoro Mahanga amesema kesi hizo zitatajwa Ijumaa mahakamani hapo, kuanzia saa tatu asubuhi.

Amesema shauri namba 6/218 lililofunguliwa na Bob Chacha Wangwe, akisimamiwa na Wakili Fatuma Karume kuhusu Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi litatajwa mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu.

Dk Mahanga amewataja majaji hao kuwa ni Jaji Wambali JK, Jaji Mwandambo J na Jaji Teemba J.

Amesema shauri namba 4/2018 lililofunguliwa na Francis Garatwa, Baraka Mwango na Allan Bujo ambao wanatetewa na Wakili Jebra Kambole kuhusu Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya vyama vya siasa litatajwa mbele ya jopo la majaji watatu ambao ni Jaji Wambali JK, Jaji Sameji R na Jaji Teemba J.

“Wananchi wapenda demokrasia ya kweli ni vema na busara kuhudhuria na kufuatilia mashauri haya yatakayokuwa yakiendelea kunguruma Mahakama Kuu, ”amesema Dk Mahanga.