Kiama cha viwanda vilivyobinafsishwa chaja

Waziri wa Viwanda na Biashara Charles Mwijage

Muktasari:

  • Awataka wanaomiliki viwanda hivyo waviachie kwa sababu wameshindwa kuviendesha

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara Charles Mwijage amesema ifikapo Agosti  15 viwanda vilivyobinafsishwa na havifanyi kazi vitachukuliwa na Serikali na kutolewa kwa wawekezaji wengine.

Akiongea na waandishi wa habari leo Alhamisi, Julai 27, Mwijage amesema Serikali haina shida na viwanda vilivyobinafsishwa na vinafanya kazi, bali uamuzi huo unavilenga ambavyo havifanyi uzalishaji kwasababu masilahi ya Serikali kwenye viwanda ni vizalishe bidhaa.

 “Wote ambao wanaviwanda vilivyobinafsishwa, lakini hivifanyi kazi au vinasuasua  wajue kwamba mwezi ujao tutafanya uamuzi wa ajabu,’’ amesema.

Ameongeza kwamba “ikiwa kiwanda kimekushinda mpe  mwingine ilimradi kifanye kazi kama siyo hivyo nitakichukua na kuwapa vijana waliotoka chuo kikuu ambao hawana ajira watakiendesha,” amesema.

Mwijage amesema kesho kutwa (Julai 29) yeye pamoja na baadhi ya wajasiriamali wanatarajia kwenda nchini Vietnam katika kongamano la kibiashara ambalo litawasaidia Watanzania kupata fursa za biashara na uwekezaji na ubia mzuri kutoka kwa wawekezaji wa nchi hiyo.