Kiama waliotajwa mali za CCM kuanza Jumatatu

Dar es Salaam. Hatima ya wana CCM waliotajwa katika ripoti ya ubadhirifu, utapeli na wizi wa mali za chama hicho huenda ikajulikana wiki ijayo baada ya vikao vya juu vilivyopangwa kufanyika Jumatatu na Jumanne.

Hatua hiyo ni baada ya mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kuahidi kupeleka ripoti ya uchunguzi wa mali hizo kwenye vikao hivyo ndani ya mwezi huu ili kuijadili na viongozi kutoa maelekezo.

Taarifa ya chama hicho kwa vyombo vya habari ilisema jana kuwa, kutakuwa na vikao vya Kamati Kuu (CC) pamoja na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) vitakavyofanyika kwa siku mbili, Mei 28 na 29.

Hata hivyo, taarifa hiyo iliyosainiwa na katibu wa NEC- Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ilisema kuwa vikao hivyo ni vya kawaida na kwamba vinaketi kwa mujibu wa ibara ya 102(2) ya katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2017.

Katika vikao hivyo, Polepole alisema NEC pia itashughulika na kazi zake zingine, ikiwamo kujaza nafasi zilizo wazi za wajumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa. Kujazwa kwa nafasi hizo kunafuatia uchaguzi wa wajumbe wa NEC uliomalizika Desemba 2017 ambapo wajumbe wanaoingia CC moja kwa moja kupitia nafasi zao walishapatikana.

Wajumbe hao ni mwenyekiti, makamu wenyeviti, wenyeviti wa jumuiya za chama (vijana, wazazi na wanawake), wajumbe wa sekretarieti (katibu mkuu, naibu makatibu wakuu na makatibu wa itikadi na uenezi; fedha na uchumi; mipango na oganaizesheni na mambo ya nje), maspika wa bunge, baraza la wawakilishi na waziri mkuu.

Kutokana na uamuzi wa chama hicho kupunguza idadi ya wajumbe kutoka 34 hadi 24, hivyo wajumbe wanaosalia kukamilisha idadi ni wanane.

Waliotajwa na kamati ya Bashiru

Wakati ikiwa ni wazi kuwa hatima ya watu waliotajwa kwenye kamati iliyochunguza wizi, utapeli na ubadhirifu wa mali za chama hicho huenda ikajulikana, wachunguzi wa masuala wa siasa wanasema uwezekano wake ni mdogo kutokana na muda mfupi wa vikao hivyo.

Hatua hiyo inafuatia ripoti ya kamati ya kuhakiki mali za chama hicho iliyoundwa na Rais Magufuli chini ya Dk Bashiru Ally kubaini upotevu mkubwa wa mali za chama uliosababishwa na mikataba mibaya, ubadhirifu, wizi, usimamizi mbaya wa mali, utapeli na ukosefu wa maadili katika uendeshaji wa miradi ya chama.

Akizungumza wakati wa kupokea ripoti hiyo mapema wiki hii, Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM alisema haiwezekani kupiga vita rushwa na ufisadi ndani ya Serikali wakati chama kina rushwa na ufisadi.

Alisema anataka pia chama kisafishwe ili mambo ya rushwa na ufisadi yaishe na Tanzania iende vizuri.

Rais Magufuli alienda mbali zaidi na kuwaagiza wajumbe wa sekretarieti ya CCM waliohudhuria hafla ya uwasilishwaji wa ripoti hiyo kuanza kufanyia kazi baadhi ya mambo yaliyo ndani ya uwezo wao na kwamba, masuala mengine yataamuliwa na vikao vya juu vya chama.

Akihutubia Mkutano Mkuu wa CCM jijini Dodoma mwanzoni mwa mwaka jana, Rais Magufuli aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa anataka kusimamia mali za chama na chini ya uongozi wake chama hicho hakitakuwa ombaomba tena.

Alisema kwa miaka yote CCM imekuwa ikiomba hata kwa watu ambao hawastahili wakati ina mali nyingi ambazo zinatumiwa vibaya na baadhi ya wanachama ambao sio waaminifu.

Kamati ya Dk Bashiru ilitangazwa Desemba 20 mwaka jana ikiwa na wajumbe tisa.

Akikabidhi ripoti hiyo, Dk Bashiru alisema uhakiki huo umefanywa kwa mali za chama hicho, jumuiya na kampuni zake.

Alisema wakati wa utekelezaji wa kazi hiyo, walitembelea maeneo yenye mali za chama hicho na kuwahoji watu mbalimbali wakiwamo viongozi waliohusishwa na mali zilizokuwa zikihakikiwa.

Dk Bashiru alisema kuwa, kamati imepitia nyaraka na kufuatilia uhalisia katika ofisi za mamlaka husika, kufanya uchambuzi wa taarifa na kutoa mapendekezo.

Maoni ya wachambuzi

Akizungumzia vikao hivyo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Beson Bana alisema hatua ya kufikisha ripoti hiyo katika vikao vya juu vya chama hicho ni sawa, ingawa haoni hatua kubwa itakayofikiwa kwa sasa kutokana na muda wa vikao kuwa mdogo.

“Huwezi kumhukumu mtu bila kumpa nafasi, vikao hivi vinakutana kwa siku mojamoja sidhani kama watapata nafasi ya kuisoma ripoti hiyo yenye volume nyingi vile nilivyoviona na wakati huohuo itoe haki sawa ya kuwasikiliza watuhumiwa kisha kutoa maamuzi,” alisema.

Hata hivyo, Dk Bana alisema dhamira ya Rais imeonekana wazi kwamba ana nia ya dhati ya kupinga ufisadi na hata katika matukio mengine kama vile ya makinikia, wafanyakazi hewa na walioghushi vyeti hakuchukua hatua mpaka pale alipounda tume kuchunguza masuala hayo.

“Nia ya dhati ipo ila wanahitaji muda zaidi. Kwanza wajumbe wenyewe wanapaswa waisome ripoti ile kwa uangalifu mkubwa kisha waliotuhumiwa wapate haki ya kujitetea kabla ya kuwachukulia hatua, kwani naamini hilo limefanyika katika tume hiyo vivyo hivyo inapaswa kufanywa na chama pia,” alisema Dk Bana.

Hatua zaidi

Mwishoni mwa mwaka jana chama hicho kilitangaza ‘kiama’ kwa wanachama wake waliojimilikisha mali za chama hicho.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Polepole alisema kwa muda mrefu mali za chama hicho zilikuwa zikimilikiwa na vikundi au watu binafsi jambo lililosababisha kukikosesha mapato.

“Nawaambia wajiandae kuanzia wiki ijayo tutaanza kubomoa nyumba za watu, yakiwamo maghorofa ambayo yalijengwa katika viwanja vya chama kwani mpaka sasa tumeshinda kesi kadhaa ambazo zinatutaka tuyarejeshe maeneo yetu.

“Kuna watu walidhani hatutawafikia katika zoezi hili ukweli ni kwamba hakuna jiwe litakalobaki bila kugeuzwa. Na huu ni mwanzo tu maafa zaidi yanakuja,” alisisitiza Polepole.

Alisema katika uhakiki huo pia wameweza kurudisha jumla ya viwanja vya michezo 22 kati ya 33 na hatua zaidi zinaendelea ili kuhakikisha mali zote za chama hicho zinarudishwa.